1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

100,000 hufa kwa dawa bandia Afrika

17 Januari 2018

Afrika inakabiliwa na changamoto kubwa ya magonjwa lakini sasa kuna changamoto kubwa zaidi ya kutibu magonjwa hayo, nayo ni dawa bandia ambazo husababisha takribani vifo vya watu 100,000 kwa mwaka. 

https://p.dw.com/p/2r1qj
Jemen Cholera-Ausbruch
Picha: Reuters/K. Abdullah

Bara la Afrika linakabiliwa na changamoto kubwa ya magonjwa lakini sasa kuna changamoto kubwa zaidi ya kutibu magonjwa hayo. Kukua kwa biashara ya dawa bandia ni janga jingine barani humo ambalo husababisha takribani vifo 100,000 kwa mwaka. 

Hakuna chochote kinachojificha kuhusiana na soko la Roxy lililoko mjini Abidjan, nchini Ivory Coast ambalo ni maarufu kwa uuzaji wa dawa bandia. Na kila mara mamlaka zimekuwa zikililenga eneo hilo na kuchoma kiasi kikubwa cha dawa bandia. Lakini wauzaji wa dawa hizo hurejea upya kila mara.

Mariam ni miongoni mwa wachuuzi wa dawa hizo, kuanzia dawa za kupunguza maumivu, antibayotiki, dawa za kutibu malaria hadi dawa za kupunguza makali ya Ukimwi, ARV, amesema polisi huwasumbua sana, lakini polisi hao hao pia ni wanunuzi wa dawa hizo.

Fatima, ambaye pia ni mchuuzi wa dawa hizo amesema, "watu wengi wanakuja hapa na vyeti vya dawa walivyoandikiwa hospitali na hununua dawa hizi, na hata wamiliki wa vituo vya afya vya binafsi pia hununua. Fatima amesema kulikuwa na genge la wafanyabiashara linalodhibiti biashara hii na huwa na mikutano ya mara kwa mara kupanga bei na kiwango cha usambazaji.

Thailand Drogen Ya-Ba Tabletten
Dawa bandia ni janga jingine kubwa zaidi barani AfrikaPicha: picture-alliance/dpa/B. Walton

Kulingana na shirika la afya ulimwenguni, WHO, dawa bandia husababisha takribani vifo 100,000 kwa mwaka barani Afrika.

Biashara hiyo haramu huingiza mapato ya asilimia 10 ya biashara ya dawa duniani, hii ikimaanisha kwamba inapata makumi kwa mabilioni ya dola kwa mwaka, makadirio haya yakiwa ni kulingana na taasisi ya jukwaa la uchumi duniani, yenye makao yake nchini Uswisi, na kuongeza kuwa kiwango hicho ni ongezeko la karibu mara tatu katika kipindi cha miaka mitano.

Biashara ya dawa bandia huingiza mapato makubwa zaidi ya biashara nyingine haramu.

Mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza na ya tropiki, ambaye pia ni mkuu wa zamani wa shirika la Msalaba Mwekundu la Ufaransa, Marc Gentilini amesema biashara ya dawa inahitaji wateja akiongeza kuwa idadi ya wagonjwa ambao ni maskini ni kubwa zaidi Afrika kuliko sehemu nyingine yoyote duniani.

Amesema baadhi ya chanjo za ugonjwa wa uti wa mgongo zilizotumwa miaka kadhaa iliyopita baada ya kuibuka nchini Niger zilikuwa bandia. Ugonjwa huo huua maelfu kila mwaka nchini humo.

Pakistan Drogenmissbrauch
Dawa bandia zinapokamatwa huteketezwa kwa kuchomwa moto kwenye mataifa mbalimbaliPicha: PID of Government of Pakistan

Who inatakadiria kwamba dawa moja kati ya 10 duniani ni bandia, lakini idadi hii inaweza kuwa ni ya juu zaidi inayoweza kufikia dawa 7 kati ya 10 kati baadhi ya nchi, hususan barani Afrika. 

Shirika la Kimarekani linalojihusisha na dawa za magonjwa ya tropiki, la American Society of Tropical Medicine and Hygiene lilikadiria kwamba mnamo mwaka 2015, watoto 122,000 walio chini ya miaka mitano walikufa baada ya kutumia dawa za malaria zilizokuwa na ubora duni katika barani Afrika, pamoja na dawa za antibayotiki ambazo zinahitajika kwa kiasi kikubwa barani humo. Dawa hizo ama hukutwa muda wake umekwisha ama ni bandia.

Polisi ya kimataifa, Intapol mnamo mwezi Agosti ilitangaza kukamata tani 420 za dawa bandia huko Afrika Magharibi wakati ilipofanya operesheni kali iliyohusisha takribani polisi 1,000, wafanyakazi wa idara ya forodha na maafisa afya kutoka nchi 7 za Benin, Burkina Faso, Ivory Coast, Mali, Niger, Nigeria na Togo.

Mkuu wa kitengo cha kupambana na dawa feki katika kiwanda cha kuzalisha dawa cha Sanofi cha nchini Ufaransa Geoffroy Bassaud amesema dawa bandia imekuwa ni biashara kubwa haramu duniani kote. Amesema "uwekezaji wa dola 1,000 unaweza kutoa faida ya hadi dola 500,000, wakati uwekezaji kama huo katika biashara ya dawa za kulevya aina ya Heroine ama fedha bandia, unaweza kutoa faida ya kiasi cha dola 20,000 tu."  

Serikali ya Ivory Coast, mnamo mwezi Mei ilichoma tani 40 za dawa bandia katika mji wa Adjame, ambao ni maarufu zaidi kwa biashara ya dawa bandia Afrika Magharibi, ambao hujumuisha asilimia 30 ya mauzo ya dawa za aina hiyo nchini Ivory Coast.

Mwandishi: Lilian Mtono/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu