ABIDJAN : Mahasimu wa Ivory Coast kukutana Afrika Kusini
26 Machi 2005Kiongozi wa waasi nchini Ivory Coast atahudhuria mazungumzo ya amani nchini Afrika Kusini wiki ijayo ambapo kwayo serikali pia itawakilishwa yumkini na Rais Laurent Gbagbo.
Mazungumzo hayo yatakuwa chini ya uwenyeji wa Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini ambaye amepewa mamlaka na Umoja wa Afrika kujaribu kufufua mchakato wa amani ulio hoi katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi iliogawika kutokana na vita.
Msemaji wa Gbagbo Desire Tagro amesema kiongozi huyo wa Ivory Coast yumkini akahudhuria mazungumzzo hayo mjini Pretoria ambayo ofisi ya Rais nchini Afrika Kusini imesema yatafanyika tarehe 3 April.
Msemaji wa waasi wanaoshikilia eneo la kaskazini ya nchi hiyo amesema kiongozi wa waasi Guillaume Soro atakuwepo kwenye mazungumzo hayo.
Magazeti ya Ivory Coast yamesema kiongozi wa upinzani Alassane Quattara ambaye kutolewa kwake katika uchaguzi wa Rais wa mwaka 2000 kunaonekana kuwa kitovu cha mgogoro huo wa Ivory Coast na Rais wa zamani wa nchi hiyo Henri Bedi pia wamealikwa na Mbeki kuhudhuria mazungumzo hayo.