1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Abiy Ahmed: Jeshi la Ethiopia limechukua udhibiti wa Mekele

29 Novemba 2020

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amesema majeshi ya nchi hiyo yamechukua udhibiti wa mji mkuu wa jimbo la Tigray, Mekelle.

https://p.dw.com/p/3lyM8
Tigray-Konflikt | Militär Äthiopien
Picha: Ethiopian News Agency/AP/picture alliance

Abiy ametangaza kuwa serikali ya shirikisho sasa imechukua udhibiti kamili wa mji huo ikiwemo uwanja wa ndege, taasisi za umma, ofisi za utawala wa jimbo hilo na maeneo mengine muhimu.

Katika ujumbe wake kupitia ukurasa wake wa Twitter siku ya Jumamosi, Abiy ametangaza pia kuwa wamemaliza operesheni yao ya kijeshi katika jimbo hilo.

Abiy ameongeza pia kuwa maelfu ya wanajeshi ambao walikamatwa na wapiganaji wa chama tawala katika jimbo hilo ‘Tigray People's Liberation Front'- TPLF, yaani Chama cha Ukombozi wa Watigray pia wameachiliwa huru. Chama cha TPLF kimekuwa madarakani katika jimbo hilo la kaskazini mwa Ethiopia.

Soma pia: Mji mkuu wa jimbo la Tigry, Mekelle washambuliwa vikali

Serikali ya Ethiopia ilianzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya TPLF zaidi ya wiki tatu zilizopita kwa lengo la kuwaondoa madarakani.

Mkuu wa majeshi nchini Ethiopia, Jenerali Birhanu Jula Gelalcha
Mkuu wa majeshi nchini Ethiopia, Jenerali Birhanu Jula GelalchaPicha: Office of the Prime Minister

Awali, ripoti katika shirika la habari linalohusishwa na serikali ya jimbo hilo zilisema mji wa Mekelle ulishambuliwa kwa makombora mazito.

Hata hivyo, jopo-kazi lililoundwa na serikali kuu kufuatilia mzozo wa Tigray, limesema hayo ni madai ya uwongo ambayo yanaenezwa na TPLF kwamba serikali serikali kuu imefanya mashambulizi dhidi ya miji na maeneo ya makaazi ya raia.

Soma pia: Guterres atoa wito wa kusitishwa mapigano Tigray, Ethiopia

Kulingana na tarifa ya serikali kuu, vikosi vya serikali vinalenga tu maghala ya silaha za kijeshi ya TPLF na kwamba wanajeshi wa serikali ya shirikisho hawajafanya mashambulizi yoyote dhidi ya miundo mbinu muhimu za raia kama hospital, shule au maeneo ya makaazi.

Taarifa hiyo imeongeza zaidi kuwa wanajeshi wa vikosi vya serikali havijafanya mashambulizi katika maeneo yenye watu wengi.

Soma pia: Abiy avitaka vikosi vya TPLF kujisalimisha ndani ya saa 72

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy AhmedPicha: DW/S. Teshome

Mnamo Jumamosi, mkuu wa majeshi wa Ethiopia Jenerali Berhanu Jula alisema baada ya vikosi vyake kuchukua udhibiti kamili wa mji wa Mekelle, sasa wanawasaka wapiganaji wa TPLF wanakojificha.

Hakukuwa na jibu la moja kwa moja kutoka upande wa TPLF.

Machafuko ya jimbo la Tigray yalianza mapema mwezi huu wakati Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2019, alipoviamrisha vikosi vyake kuanza operesheni kwa lengo la kuuondoa uongozi wa jimbo la Tigray.

Chama cha TPLF kimetawala siasa za Ethiopia kwa miaka mingi, lakini tangu Abiy Ahmed alipochukua madaraka mnamo mwaka 2018, amekuwa na msuguano na viongozi wa Tigray.

Pande zote mbili zimeripoti kuhusu mauaji lakini kufuatia kuzimwa kwa intaneti pamoja na huduma za mawasiliano ya simu kukatizwa, imekuwa vigumu kupata tarifa kamili ya vifo kuhusiana na machafuko hayo ya Tigray, ikiwa ni pamoja na mashambulizi kadhaa ya angani na kisa kimoja cha mauaji ya halaiki ambapo mamia ya watu waliuawa.

Mamia ya watu wameripotiwa kuuawa na zaidi ya Waethiopia 40,000 wamekimbia vita na kuingia Sudan.

(DPAE, AFPE)