AFCON 2013 : Sare yatawala
20 Januari 2013Tamasha la soka la 29 katika bara la Afrika ambalo limekuwa likisubiriwa kwa hamu kubwa, ambalo lilianza katika mazingira ya dhalili mwaka 1957 na kuwa tukio linaloleta mvuto duniani kote , lilianza kwa sare ya bila kufungana katika mchezo dhaifu baina ya wenyeji Afrika kusini Bafana Bafana na timu iliyopata nafasi kwa mara ya kwanza kuingia katika kinyang'anyiro hicho Cape Verde.
Mchezo huo wa kwanza wa ufunguzi ulifuatiwa na mchezo bora zaidi baina ya Morocco na Angola katika uwanja huo huo lakini pia ukamalizika kwa sare ya bila kufungana.
Kocha afurahi
Watu pekee ambao walionekana hasa kuridhika na siku ya kwanza ya fainali hizo, ambapo wengi watapendelea kuisahau haraka , ni kocha wa Cape Verde Lucio Antunes na kikosi chake.
Amefurahishwa na ukweli kwamba wamemaliza mchezo huo kwa imani ya kweli kwamba wanaweza kupata matokeo zaidi mazuri dhidi ya Morocco na Angola katika michezo yao iliyobaki katika kundi A na kuepuka kurejea nyumbani na mapema.
"Kwangu mimi ilikuwa kazi iliyokamilika," amesema Antunes. "Kikosi changu kilikuwa safi kabisa, tulifanya kazi tuliyokuja kuifanya na tumekamilisha matarajio yetu na sasa tunaweza kuelekeza mawazo yetu katika mchezo ujao dhidi ya Morocco.
"Nina furaha , wachezaji wanafuraha na benchi la ufundi limefurahi. Leo tumeipa hadhi nchi yetu. Ni nchi ndogo ya visiwa yenye wakaazi 500,000, lakini leo tumewafanya wajisikia fahari.
Afrika kusini yainamisha kichwa
Kocha wa Afrika kusini Gordon Igesund ana mtazamo mwingine kabisa baada ya pambano hilo lililodorora, lililojaa makosa kadha lililochezwa katika mazingira ya baridi kama wakati wa majira ya baridi huku mvua ikinyonyota katika uwanja huo.
Hata hivyo hali hiyo haikuweza kuzuwia matarumbeta ya Vuvuzela kuhanikiza uwanjani, kelele zake ambazo mara nyingine hazivumiliki zinatoa burudani kwa watazamaji katika michezo ya soka nchini Afrika kusini.
"si wachezaji wengi walikuwapo katika tamasha hili katika nusu ya kwanza , na hatukuwa katika hali nzuri katika kipindi cha pili," Igesund amewaambia waandishi habari baada ya kile ambacho kilikuwa mchezo mbovu wa ufunguzi wa mashindano haya ambao ulionekana moja kwa moja katika televisheni na mamilioni ya watu duniani kote.
"Baadhi ya wachezaji walionekana kama wameganda wakati firimbi ya mwisho ilipolia , walionekana kuwa hawajiamini. pengine kwa baadhi yao tukio hilo lilikuwa kubwa mno, ameongeza kocha Igesund.
Leo (20.01,2013) ni zamu ya Ghana ikitiana kifuani na jamhuri ya kidemokrasi ya Congo, na baadaye Mali itaonyeshana kazi na Niger.
Mwandishi : Sekione Kitojo
Mhariri : Stumai George