AFCON 2013: Ukame wa magoli waisha
21 Januari 2013Michuano ya kuwania ubingwa wa mataifa ya Afrika , AFCON 2013, imezinduka na kupata uhai jana Jumapili , kwa timu kuweza hatimaye kupata magoli . Ushindi pamoja na ishara ya hazina ya kandanda ambalo linaweza kuonekana baadaye katika mashindano haya yatakayochukua muda wa wiki tatu , zimeonekana kufuatia mwanzo ambao ni wa kudorora wa michuano hiyo ulioonekana siku ya Jumamosi(19.01.2013).
Miongoni mwa hazina hizo ni pamoja ushangiliaji wa kipa wa jamhuri ya kidemokrasi ya Congo Robert Kidiaba.
Magoli yameonekana , matatu katika michezo matatu katika kipindi cha pili , wakati kikosi cha jamhuri ya kidemokrasi ya Congo kilipopambana kiume kutoka kuzabwa mabao 2-0 na Ghana na hatimaye kutoka sare ya mabao 2-2 katika uwanja wa Nelson Mandela Bay mjini Port Elizabeth.
Hata hivyo hiyo ilikuwa sare ya tatu katika michezo mitatu iliyokwisha chezwa , kufuatia sare ya bila kufungana baina ya kikosi cha Afrika kusini Bafana Bafana na Cape Verde na halikadhalika Morocco ilipotiana kifuani na Angola.
Licha ya kuwa magoli yamekuwa kama matone ya maji katika msimu huu wa michuano ya kombe la mataifa ya Afrika wakati Mali ilipochuana na Niger jana Jumapili, mchezaji wa zamani wa Barcelona Seydou Keita hakusita kupachika bao pale ilipotokea fursa katika dakika ya 84 ya mchezo huo ambao hata hivyo ulikuwa wa taratibu mno na mbinu za kulinda lango zaidi ya kushambulia kwa upande wa Niger.
Huenda mambo yakabadilika na kuonesha uhai zaidi katika michuano hii wakati mabingwa watetezi Zambia watakapoingia uwanjani leo jioni kupambana na Ethiopia , timu pekee kutoka ukanda wa Afrika mashariki. Mchezo huo utafuatiwa na pambano lingine baina ya Nigeria na Burkina Faso.
Lakini pia hapo kesho(22.01.2013) kutakuwa na patashika nyingine , wakati majirani wa eneo la maghreb Tunisia na Algeria watakapooneshana kazi , katika pambano ambalo linaonekana litakuwa la kuvutia, ikiwa ni mara yao ya kwanza kupambana katika mashindano haya.
Kocha wa Algeria Vahid Halilhodzic ameazimia katika pambano hili la kundi D kuwa ni lazima kupata ushindi , wakati timu aliyokuwa akiifunza kabla ya Cote D'Ivoire ikitarajiwa kushika nafasi ya kwanza katika kundi hilo. Algeria inatabiriwa kuwa moja kati ya timu ambazo zinaweza kuonyesha uwezo mkubwa katika mashindano haya ya AFCON 2013.
Didier Drogba akiwa na Tembo la Cote D'Ivoire wanapigiwa upatu kulinyakua taji la ubingwa wa mataifa ya Afrika msimu huu na wanatarajiwa kuwaweka kando Togo kirahisi katika mchezo wao kesho jioni(22.01.2013).
Kwa Didier Drogba mwenye umri wa miaka 34, akiwa mchezaji maarufu zaidi katika bara la Afrika kwa sasa , hii ni fursa yake ya mwisho hatimaye kuongeza taji hilo katika mkusanyiko wake mkubwa wa mataji aliyoyapata katika mashindano mbali mbali.
Ligi barani Ulaya,
Bayern Munich ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Greuther Feurth na kuweza kulinda uongozi wao wa points tisa wakati ligi ya Bundesliga iliporejea tena uwanjani baada ya mapunziko ya mwezi mmoja.
Mabingwa watetezi Borussia Dortmund imewasambaratisha wenyeji wao Werder Bremen siku ya jumamosi kwa ushindi wa mabao 5-0, kwa mchezo safi wa ushambuliaji na kuthibitisha kuwa bado wamo katika mchakato wa kusaka ubingwa , licha ya kuwa nyuma kwa points 12 kutoka Bayern Munich na ikiwa inashikilia nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi.
Bayer Leverkusen inashikilia bado nafasi ya pili, na ilipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Eintracht Frankfurt siku ya Jumamosi.
Jana Jumapili FC Nürnberg ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Hamburg Sportverein katika mchezo ambao ulikuwa hauna msisimko. Mchezaji wa pembeni wa Hamburg SV Marcell Jansen ameueleza mchezo huu kama hivi.
"Kimsingi kipindi cha kwanza tunaweza kusema, kilikuwa si kibaya sana. Kwa upande wa kipindi cha pili, tunaweza kusema, tumepoteza points mbili. Tuliweza kucheza mchezo mzuri zaidi".
Fortuna Dusseldorf ilikubali kipigo cha mabao 3-2 dhidi ya FC Augsburg katika mchezo uliofanyika jana Jumapili.
Huko Uhispania Atletico Madrid na majirani zao katika jiji hilo Real Madrid walichukua fursa adimu ya kushindwa kwa mara ya kwanza kwa viongozi wa ligi hiyo Barcelona kwa kupata ushindi dhidi ya Levante na Valencia kila moja jana Jumapili(20.01.2013)
Barca iliteleza baada ya kuwa mbele kwa mabao 2-0 dhidi ya Real Sociedad na kukubali kipigo cha mabao 3-2, licha ya kuwa Lionel Messi alifanikiwa kupachika bao katika mchezo wa kumi mfulilizo katika La Liga na kufikisha rekodi iliyowekwa na mshambuliaji Ronaldo katika La Liga katika msimu wa mwaka 1996-97.
Huko Uingereza Tottenham Hotspurs ilipata bao la kusawazisha katika dakika za majeruhi baada ya kupeleka mashambulizi bila kukata tamaa katika goli la Manchester United na kupata sare ya bao 1-1 na viongozi hao wa Premier League.
Nae David Silva alipachika mabao yote ya Manchester City katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Fulham. Chelsea iliifanikiwa kupata ushindi katika kile kinachojulikana London Derby, ilipoilaza Arsenal kwa mabao 2-1.
Mabingwa ambao ni watetezi wa Serie A , ligi ya Italia Juventus Turin waliisambaratisha Udinise kwa mabao 4-0 wakati Napoli na Lazio zote ziliambulia sare. Juve inaongoza kwa points 5.
Nchini Ufaransa Zlatan Ibrahimovic ameirudisha kileleni mwa ligi daraja la kwanza Paris St German baada ya ushindi bao 1-0 dhidi ya Girondins Bordeaux. Paris St. Germain inafungana kwa points na Olympique Lyon lakini inaipiku kwa magoli.
Mwandishi: Sekione Kitojo/rtre/afpe
Mhariri: Mohammed Khelef