Africa mwaka 2021: Mizozo ya kisiasa itaendelea?
COVID-19, uchaguzi, mizozo na ukanda mkubwa kabisa huru wa kibiashara ulimwenguni: DW inaelezea masuala muhimu yanayolikabili bara la Africa kwa mwaka 2021.
Ukanda mkubwa kabisa huru wa kibiashara duniani kufunguliwa Afrika.
Mwaka mpya wa 2021, mataifa ya Afrika yataingia kwenye enzi mpya kwa kuanzisha ukanda huru wa kibiashara barani humo, AfCTA. Miezi na miaka ijayo itashuhudia kuanzishwa kwa ukanda huo mkubwa kabisa wa kibiashara ulimwenguni. Wataalamu wanasema makubaliano hayo ya umuhimu mkubwa, lakini janga la COVID-19 limefanya uetekelezaji wake kuwa mgumu.
Vuta nikuvute nchini Uganda.
Operesheni za kijeshi dhidi ya upinzani- pamoja na wakosoaji na waandamanaji, vimesababisha vifo vingi. Picha za kampeni za kampeni za uchaguzi nchini humo zimeibua wasiwasi mkubwa kote ulimwenguni. Januari 14, raia watachagua kati ya rais wa muda mrefu Yoweri Museveni na msanii wa zamani Robert Kyagulanyi ama Bobi Wine. Wafuatiliaji wamesisitiza umuhimu wa kufanyika uchaguzi huru na haki.
Ni mwaka wa mustakabali kwa Upembe wa Afrika.
Je Ethiopia itaweza kushikamana tena baada ya mashambulizi mabaya ya serikali dhidi ya jeshi la ukombozi wa watu wa Tigray, TPLF? Ama taifa hilo litagawanywa na mzigo wa mizozo yake ya ndani? 2021 inaweza kuamua iwapo waziri mkuu Abiy Ahmed anaweza kufanikiwa kuleta usawa wa kidemokrasia nchini humo. Uchaguzi iliopangwa kufanyika Juni 5 huenda ukawa fursa yake muhimu kabisa.
Mizozo ya wakimbizi.
Athari moja ya mzozo wa Tigray iko wazi. Maelfu ya raia wamelikimbia jimbo hilo linalokabiliwa na matatizo lililo jirani na Sudan, ambako serikali changa inapambana kuwasaidia. Kwingineko, kuna wasiwasi kwamba mizozo inayoendelea itasababisha mizozo mipya ya wakimbizi ilihali ya awali bado haijasuluhishwa. 2021 utakuwa ni mwaka mwingine mgumu nchini Cameroon, kaskazini mwa Nigeria na DR Congo.
Uchaguzi mgumu ujao.
Uganda pamoja na Ethiopia, Benin, Somalia, Sudan Kusini, Cape Verde, Chad na Gambia watafanya uchaguzi mwaka huu wa 2021 kuchagua viongozi wapya. Wakati baadhi ya mataifa yakitarajia uchaguzi usio na usawa, hali nchini Somalia na Sudan Kusini tayari ni ya kutia wasiwasi kutokana na mazingira tete ya kiusalama.
Matumaini ya upatikanaji wa chanjo ya COVID-19
"Ingawa mataifa ya Afrika yako pazuri katika janga la COVID-19 kuliko ilivyotarajiwa, athari za kiafya na kiuchumi bado ni kubwa. Matarajio ya chanjo ni makubwa, lakini Afrika haiko tayari kwa kampeni kubwa ya chanjo ambayo haijashuhudiwa," alisema Matshidiso Moeti, wa shirika la WHO. Wataalamu hawatarajii chanjo kuanza hadi katikati ya 2021 kutokana na ugumu wa upatikanaji wa vifaa.
Je kutarajiwe unafuu wa madeni?
Moja ya athari za janga la corona ambayo haitaondoka kwa urahisi hata baada ya upatikanaji wa chanjo: Baadhi ya mataifa ya Afrika yamefilisika. Ingawa mataifa yaliyostawi kiuchumi ulimwenguni ya G20 yalianzisha mpango wa kupunguza madeni, asasi siziso za kiserikali hivi sasa zinatoa mwito wa kupunguzwa kwa kiasi kikubwa madeni hayo ili pia kupunguza athari za kibinadamu za COVID-19.
Mzozo unaonyemelea wa mazingira.
Ukame, janga la nzige, mafuriko: Hakuna bara linaloathirika pakubwa na mzozo wa kimazingira kama Afrika. Lakini wanaharakati chipukizi kama Vanessa Nakate wa Uganda hawataki tena msaada wa wa mataifa tajiri. Anapambania barala la Afrika kusikilizwa katika majukwaa ya kiulimwengu na atakuwa mmoja wa mwakilishi na mkosoaji mkubwa kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mazingira Novemba 2021.