Afrika katika magazeti ya Ujerumani:Jino la Lumumba larejea
24 Juni 2022Gazeti la Süddeutsche lililokuwa na kichwa cha habari "Jino moja tu linarejea." Mabaki ya waziri mkuu wa kwanza wa Congo Patrice Lumumba yamerejeshwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Waliweka bendera ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo juu ya jeneza, katika kiwanja cha ikulu ya Egmont mjini Brussels siku ya Jumatatu asubuhi. Wanajeshi wakasimama kuyalinda, bendi ikacheza wimbo wa taifa wa Congo. Kwenye skrini kubwa kukawa na picha ya Patrice Lumumba, aliyeuliwa miaka 61 iliyopita lakini hakuwahi kuzikwa katika miongo yote hiyo kwa sababu kwa muda mrefu hakukuwa na kitu cha kumfanyia mazishi. Sasa angalau kuna jino moja lililowekwa kwenye jeneza kubwa, kwenye kisanduku kidogo kilichotengenezwa kwa mkono na kupakwa rangi nyeupe.
Aliyesimama mbele ya jeneza hilo ni waziri mkuu wa Congo, Jean-Michel Sama Lukonde na mwenzake wa Ubelgiji, Alexander De Croo. Mhariri alimnukuu Croo akisema "Ningependa kuoamba radhi hapa mbele ya familia yake, kibinafsi, kwa jinsi serikali ya Ubegiji ilivyoshawishi uamuzi wa kuyakatisha maisha ya waziri mkuu wa kwanza wa Congo". Ni kauli ambayo familia ya Lumumba haijawahi kuisikia hapo kabla ikitolewa namna hiyo, ambayo wameisubiri kwa muda mrefu sana.
Gazeti la Die Welt nalo liliandika kuhusu jinsi jino moja linavyotakiwa kusaidia kuleta maridhiano na Congo. Ubelgiji inakabiliwa na mtihani mgumu kukabiliana na historia yake ya ukoloni na sasa imerejesha mabaki ya mpigania uhuru wa Afrika Patrice Lumumba. Nchi moja pamoja na watu wake wote kama mali ya wakoloni wake, raslimali zake zikitumiwa kwa msaada wa utumwa na ugaidi. Mhariri anasema hadi leo Ubelgiji inajizatiti kuikubali hali halisi ya historia yake ya ukoloni, na msamaha rasmi kwa watu wa Congo, taifa la pili kwa ukubwa barani Afrika, haujatolewa. Lakini sasa jino moja tu ndilo linalotazamiwa kuboresha na kuimarisha mahusiano yaliyovurugika kati ya Congo na Ubelgiji.
Mkutano wa CHOGM wafanyika Kigali
Mada nyingine iliyozingatiwa na wahariri wiki hii ni mkutano wa nchi za Jumuiya ya Madola mjini Kigali, Rwanda. Gazeti la Die Welt liliandika: Mkutano wa kilele wenye hisia maalumu. Rwanda ni nchi ya kwanza ambayo haikuwa koloni la Uingereza kuandaa mkutano wa nchi za Jumuiya ya Madola. Lakini ongezeko la hali ya wasiwasi na kudorora kwa usalama katika eneo la mpaka na nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inasababisha matatizo. Mhariri wa gazeti la Die Welt aliandika kuwa matukio mbalimbali yaliyoandaliwa kwenye mkutano huo yalianza tangu Jumapili iliyopita mjini Kigali katika mazingira ya usalama kuimarishwa.
Mkutano wa CHOGM 2022 ni wa kwanza kwa mrithi wa ufalme wa Uingereza na Rwanda. Si tu wa kwanza kuandalwia nchini Rwanda, bali pia ni kwanza kufanyika katika nchi ambayo haikuwa koloni la Uingereza. Hali hii imeipa hisia maalumu mkutano huo wakati waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson na Mwanamfalme Charles walipojiunga na mkutano huo. Wajumbe 5,000 walikusanyika katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali ambako mkutano huo ulianza Jumapili iliyopita kwa kongamano la vijana. Mkutano huo ulitakiwa kufanyika tangu 2020 lakini ukaahirishwa kutokana na janga la corona.
Ramaphosa abanwa Afrika Kusini
Gazeti la Frankfurter Allgemeine lilikuwa na kichwa cha habari kilichosema: Ramaphosa mashakani. Mhariri wa gazeti hilo aliandika kwamba rais huyo wa Afrika Kusini anakabiliwa na shikinizo kuhusiana na wizi wa kisiri katika shamba lake la wanyamapori. Nyavu za wachunguzi zimeanza kumbana rais Cyril Ramaphosa katika kashfa kubwa ya rushwa Afrika Kusini tangu kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi. Ripoti ya tano na ya mwisho ya tume ya uchunguzi ya jaji mkuu Raymond Zondo ilitarajiwa kuwasilishwa kwa rais Ramaphosa katika shughuli rasmi Jumatatu iliyopita. Kazi ya tume hiyo ilichukua miaka minne, mamia kadhaa ya mashahidi walihojiwa na kusikilizwa na kiasi kikubwa cha data kilikusanywa.
Ripoti hiyo inaelezea jinsi akina Gupta, familia rafiki ya wafanyabiashara na rais wa zamani Jacob Zuma, na wengine walivyofanikiwa kupora fedha kutoka kwa makasha ya serikali na kuziendesha karibu tasisi zote za serikali kinyemela nyuma ya pazia. Baada ya ripoti kuwasilishwa kinachosubiriwa ni kesi kufunguliwa na wahusika kuwajibishwa mbele ya vyombo vya sheria na hukumu kutolewa.
Sadio Mane atinga timu Bayern Munich
Tunakamilisha na taarifa ya gazeti la Frankfureter Allgemeine lililoandika kuhusu ujio wa mchezaji wa timu ya taifa ya Senegal, Simba wa Teranga, Sadio Mane, katika Bundesliga. Mhariri alisema Mane ni mchezaji aliyekamilika, anayechanganya mbinu zote zinazomfanyaka kuwa mshambuliaji hatari mwenye uwezo mkubwa wa kufunga magoli. Mhariri aliendelea kuandika kwamba kuwasili Mane mjini Munich na kusaini mkataba wa miaka mitatu na mabingwa Bayern Munich, akitokea klabu ya Liverpool katika ligi ya Premier, ni tukio la mapinduzi makubwa sio tu kwa Bayern bali kwa ligi nzima ya kandanda ya Ujerumani, Bundesliga.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 ni miongoni mwa nyota wa soka duniani anayeweza kupata nafasi katika timu yoyote. Ujio wake unaisaidia ligi ya Bundesliga ambayo imekuwa ikigubikwa na ligi ya Premier, na kurejesha hamasa ambayo pengine ilipotea baada ya kuondoka mshambuliaji wa klabu ya Borussia Dortmund Erling Haaland aliyetimkia Manchester City na pengine uwezekano wa kuondoka kwa mshambuliaji wa Bayern, Robert Lewandowski.
(Inlandpresse)