Afrika katika magazeti ya Ujerumani
21 Aprili 2013Gazeti la" Süddeutsche" linamkumbuka Albert Schweitzer.
Jee yeye alikuwa nani na kwa nini gazeti hilo linamkumbuka ?
Albert Schweitzer alikuwa daktari, mwanafalsafa na mmishonari.
Miaka 100 iliyopita, Albert Schweitzer aliekuwa Mjerumani na Mfaransa, alifunga safari kuenda Afrika. Alipowasili katika nchi ambayo leo ni Gabon alijenga hospitali inayoitwa Lamberene ambayo ni maarufu hadi leo.
Mara tu baada ya kuwasili Gabon, aliwakuta wagonjwa wa malaria ,malale na hata ukoma. Aliwatibu wagonjwa hao kwa kutumia, dawa na vifaa alivyovinunua kwa fedha zake na michango ya watu wengine.
Falsafa yake:
Albert Schweitzer alisema kila binadamu anapaswa kumsaidia mwanadamu mwenzake. "Hata ikiwa ni kwa kitu kidogo tu,kifanye kwa mwanadamu mwenzako anaehitaji msaada"
Gazeti la "Süddeutsche" linakumbusha kwamba Albert Schweitzer aliwasaidia wagonjwa hadi mwaka wa 1965 nchini Gabon. Sababu ya gazeti la Süddeutsche Zeitung" kumkumbuka daktari huyo ni kwamba sasa pana mipango ya kujenga chuo cha tiba kisichoeleweka vizuri mahala ambapo ameijenga hospitali ya Lambarene.
Misaada ya Waislamu:
Gazeti la "Neues Deutschland" wiki hii limeandika juu ya mkutano uliofanyika Florida Marekani kujadili misaada ya maendeleo inayotolewa na mashirika na nchi za kiislamu.
Gazeti hilo, limehoji kwamba jambo muhimu ni msaada unaotolewa,na siyo dini ya mhisani anaeutoa msaada.Gazeti hilo linatilia maanani kwamba msaada unaotolewa barani Afrika na mashirika ya kiislamu umekuwa unaongozeka katika miaka ya hivi karibuni.
Gazeti la "Neues Deutschland" linaeleza kuwa mkutano uliofanyika kwenye chuo kikuu cha Florida ulijadili mchango wa misaada ya mashirika ya kiislamu barani Afrika kwa kuuliza jee misaada hiyo inaleta nini barani Afrika na vipi inatofautiana na ile ambayo imekuwa inatolewa hadi sasa na jumuiya nyingine ?
Kinara wa mihadarati:
Gazeti la "Süddeutsche" pia linaarifu juu ya mkasa wa Meya wa mji mdogo nchini Mali. Gazeti hilo linatufahamisha kwamba Meya huyo, Baba Ould Sheikh wa mji wa Tarkint amekamatwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika na biashara ya dawa za kulevya. Kwa mujibu wa gazeti la "Süddeutsche" kukamatwa kwa Meya huyo ni pigo kubwa dhidi ya biashara ya mihadarati, kwani yeye ndiye kiunganisho wa biashara hiyo kati ya Ulaya na Amerika ya Kusini.
Hata hivyo gazeti la "Süddeutsche" limeripoti kwamba, licha ya kukamatwa kwa Meya huyo anaezingatiwa kuwa muhimu sana katika biashara ya mihadarati nchini Mali,na katika Afrika magharibi kwa jumla biashara hiyo inaendelea.
Biashara ya Mabilioni:
Gazeti la Süddeutsche" limenukuu takwimu za kitengo cha Umoja wa Mataifa,UNODC, kinachopambana na uhalifu wa mihadarati duniani. Kwa mujibu wa takwimu za kitengo hicho, biashara ya mihadarati thamani ya dola zaidi ya Bilioni moja kila mwaka inafanyika kwa kupitia nchini Mali na nchi nyingine za Afrika magharibi. Dawa hizo za kulevya zinasafirishwa na kupelekwa barani Ulaya kutokea nchini Mali.
Highway 10
Katika taarifa yake gazeti la Süddeutsche" pia linafahamisha juu ya njia inayoitwa Highway 10. Hilo ni jina linalotumiwa na idara za Marekani na za Ulaya, zinazopambana na biashara ya dawa za kulevya, zinapozungumzia njia ya baharini inayotumiwa na wauza unga, kusafirisha mizigo yao ya kifo.
Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen:
Mhariri: Mohammed Khelef