Ugaidi waenea Afrika
22 Januari 2016Aliekuwa Rais wa Burundi Sylvestre Ntibantunganya amesema katika mahojiano na gazeti la "die tageszeitung" kwamba Burundi inahitaji usalama kwa ajili ya wananchi wake wote na ndiyo sababu majeshi ya Umoja wa Afrika yanapaswa kupelekwa katika nchi hiyo.
Rais wa zamani wa Burundi bwana Ntibantunganya ameliambia gazeti la "die tageszeitung kwamba utawala wa Nkurunziza unapaswa kukubali kufanya mazungumzo na wapinzani .Na ameutaka Umoja wa Afrika uchukue kila hatua ili kuepusha hali kama ile iliyotokea nchini Burundi katika miaka ya nyuma.
Gazeti la "Süddeutsche" wiki hii limeandika juu ya mashambulio ya kigaidi yaliyotokea Ouagadougou, mji mkuu wa Burkina Faso. Watu karibu 30 waliuawa kutokana na mashambulio hayo.
Gazeti hilo linaeleza kwamba magaidi walizilenga sehemu zinazotembelewa na watalii wa kimataifa ili dunia nzima ijue kwamba Burkina Faso pia inaweza kushambuliwa. Hadi sasa nchi hiyo imekuwa tulivu na magaidi wamekuwa wanafanya mauaji katika nchi nyingine za Afrika magharibi kama vile Nigeria,Mali na Niger.
Gazeti la "Süddeutsche" limemnukulu Rais Roch Marc Kabore wa Burkina Faso akisema, lengo la magaidi ni kuzikwamisha juhudi za watu wa Burkina Faso za kujenga demokrasia.
Gazeti la "Der Tagesspiegel" linasema bara la Afrika limo katika hatari kutokana na kuenea kwa ugaidi.Linauliza jee bara la Afrika limegeuka uwanja wa gwaride wa Waislamu wenye itikadi kali?
"Der Tagesspiegel" linaeleza kuwa Ujerumani ina wasi wasi mkubwa juu ya kusmbaratika kwa Libya kunakosababisha vurumai kaskazini mwa Afrika. Hivi karibuni magaidi walifanya mashambulio nchini Mali na Burkina Faso.
Gazeti la "Der Tagesspiegel" linasema magaidi wanaoitwa dola la kiislamu wanaitumia Libya kama ngome ya kujitandazia kaskazini na magharibi mwa Afrika. Gazeti hilo limemnukulu Waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Ursula von der Leyen akitahadharisha kwamba, Waislamu wenye itikadi kali wanajenga nguzo ya ugaidi kaskazini mwa Afrika. Lakini ameahidi kuwa Ujerumani itatoa mchango wake katika juhudi za kuwazuia magaidi.
Gazeti la " Süddeutsche" wiki hii pia limeandika juu ya maafa yanayosababishwa na hali ya hewa inayoitwa El Nino. Gazeti hilo linasema watu zaidi ya Milioni 20 kusini na mashariki mwa Afrika wanahitaji msaada baada ya kukumbwa na athari zinazotakana na hali ya hewa ya El Nino.
Gazeti la "Süddeutsche" linafahamisha kwamba, wakati El Nino imesababisha mafuriko katika sehemu nyingine za dunia,imeleta ukame mbaya sana katika sehemu kadhaa za Afrika. Gazeti hilo linakumbusha kwamba ukame kama huo ulileta njaa iliyosababisha vifo vya watu zaidi ya Milioni moja kwenye pembe ya Afrika mnamo mwaka wa 1984.
Gazeti la "Süddeutsche" linatahadharisha kwamba,kutokana na mvuno finyu sana,kutokana na ukame, tayari watu Milioni 14 wamo katika hatari ya kukumbwa na njaa kusini mwa Afrika. Gazeti la "Süddeutsche" linafahamisha katika makala yake kwamba nchini Ehtiopia watu Milioni 10 watategemea msaada wa chakula mnamo mwaka huu.
Gazeti hilo limemnukulu makamu mwenyekiti wa baraza la wakimbizi nchini Norway akisema kwamba maafa makubwa yanainyemelea Ethiopia.Makamu mwenyekiti huyo Gier Olav Lisle hivi karibuni alifanya ziara nchini Ethiopia. Na amenukuliwa akisema kuwa mafanikio makubwa yaliyofikiwa nchini humo yamo katika hatari ya kurudi nyuma kutokana na athari za ukame.
.Mwandishi: Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen
Mhariri: Mohammed Khelef