Afrika katika magazeti ya Ujerumani
11 Januari 2019die tageszeitung
Gazeti la die tageszeitung linasema katika maoni yakelinasema kutangazwa kwa kiongozi wa upinzani Tshisekedi kuwa mshindi wa uchaguzi maana yake ni kushuhudia mabadiliko ya uongozi yaliyofanyika kwa njia ya kidemokrasia.
Gazeti hilo limeandika: Itakuwa fursa ya kihistoria, ya kulipeleka bara la Afrika mbele endapo Felix Tshisekedi kweli atakuwa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Yumkini ingeliwezekana kwa Kongo kuondokana na kizungumkuti cha migogoro na umwagikaji damu hali ambayo imeiandama nchi hiyo yenye karibu watu miloni 90 kwa muda wa miaka mingi.
Inaaminika kwamba ushindi wa Tshisekedi ni wa udanganyifu. Kulingana na kile kinachoaminiwa na watu wengi nchini Kongo mshindi wa kweli ni kiongozi mwengine wa upinzani Martin Fayulu na zipo hoja zenye mashiko juu ya madai hayo. Gazeti la die tageszeitung linasema Fayulu ni mgombea aliyekuwa anawakilisha maslahi ya wapinzani wa Joseph Kabila wanaoishi nje ya nchi.
Neue Zürcher
Nchini Gabon gazeti la Neue Zücher limeandika juu ya jaribio la kuiangusha serikali lililofanywa na wanajeshi waasi na linatuambia kwamba kikundi cha askari kilijaribu kutwaa mamlaka nchini humo kwa kusoma tamko kwenye kituo cha radio ya taifa, la kuwataka wanajeshi na wananchi kwa jumla wajiunge na njama za askari hao za kuiangusha serikali. Askari hao walipanga njama zao wakati rais Ali Bongo akiwa nje kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya maradhi ya kiharusi yaliyompata wakati akiwa nchini Saudi Arabia. Hata hivyo gazeti hilo la Neue Zücher linatilia maanani kwamba jaribio la askari hao liligunduliwa na kuzimwa.
Askari wawili waasi waliuliwa na wengine watatu walikamatwa. Gazeti la Neue Zücher linatueleza mambo yanayoweza kusababisha hatua iliyochukuliwa na askari hao waasi. Kwa baadhi ya watu, nchini Gabon, Ali Bongo si mzaliwa wa nchi hiyo. Yeye ana asili ya Nigeria. Alichukuliwa kutoka Nigeria wakati wa vita vya Biafra na kulelewa nchini Gabon na kwa hivyo kama mgeni hastahili kuwa mkuu wa nchi. Suala hilo linaendelea kuzingatiwa na mahakama mbalimbali za nchini Gabon na Ufaransa. Gazeti hilo la Neue Zücher pia linasema ukoo wa Bongo umetawala Gabon kwa muda wa miaka mingi na umelimbikiza kiasi kikubwa sana cha mali wakati thuluthi moja ya wananchi wanaishi katika umasikini.
Naam msikilizaji sasa tunaigeukia Sudan ambako rais wa nchi hiyo Omar al-Bashir anapanda jukwaani na kunengua wakati maandamano makubwa ya kumpinga yanazidi kupamba moto. Gazeti la Süddeutsche linatueleza zaidi:
NARR: Kwa muda wa wiki kadhaa sasa, maalfu ya watu nchini Sudan wamekuwa wanafanya maandamano ya kumpinga rais Omar al-Bashir alieingia madarakani kwa mabavu tangu mwaka 1989. Katika kila pembe ya nchi watu wanajitokeza kumpinga al -Bashir. Hii si mara ya kwanza kwa rais huyo kupingwa na maaflu ya watu barabarani lakini wakati wote alikuwa na majawabu. Aliwatia ndani wapinzani, aliwanunua na kuwashirikisha katika serikali yake na mara nyingine alipunguza bei ya mahitaji muhimu ili kuwaliwaza wananchi.
Süddeutsche Zeitung
Gazeti hilo linasema safari hii watu wanaompinga al -Bashir ni wengi sana. Sasa hana njia nyingine ila kupanda jukwaani na kuyatikisia mbali matatizo kwa kunengua. Gazeti la Süddeutsche linatueleza chanzo cha matatizo hayo kwamba ghasia za hivi karibuni zilianza mwishoni wa mwezi Novemba baada ya serikali kupunguza ruzuku kwa ajili ya kufidia bei za unga wa ngano na mafuta ya petroli.
Uamuzi huo ulisababisha kuongezeka kwa bei ya mkate mara nne lakini uamuzi wa serikali wa kupunguza ruzuku ulitokana na masharti ya shirika la fedha la kimataifa IMF ili Sudan ipatiwe mkopo na shirika hilo. Serikali ya al- Bashir imepungukiwa fedha. Tangu kujitenga kwa Sudan Kusini, serikali ya al-Bashir imepoteza nusu ya mapato yaliyotokana na mauzo ya mafuta yaliyoko Sudan Kusini.
Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen
Mhariri: Mohammed Khelef