1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Kusini kuwahusisha raia wake katika uwezo wa ki uchumi

26 Aprili 2005

Wakati kampuni kubwa la bima nchini Afrika Kusini la Old Mutual lilipouza sehemu ya kampuni hilo kwa watia hisa waafrika wiki iliyopita, Majina ya watu maarufu katika biashara hiyo hayakutajwa.

https://p.dw.com/p/CHh0

Kampuni hilo linasema takriban asilimia 40 ya hisa zitakwenda kwa watumishi, hatua ambayo itawahusu watu nusu milioni wa Afrika Kusini.

Hii ni hatua kubwa nchini humo inayotoa uwezo wa kiuchumi kwa watu wa Afrika Kusini.

Miaka kumi na moja baada ya kumalizika siasa za ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini biashara nyingi kubwa kubwa zingali zinamilikiwa na wazungu. Na sera ya Afrika kusini ya kuwapa uwezo wa kiuchumi waafrika weusi yaani BEE ina lenga kuhamishia utajiri na uchumi zaidi wa nchi hiyo kwenye mikono ya waafrika walio wengi nchini humo.

BEE imekuwa kama nguzo ya sera ya kiuchumi ya Afrika Kusini tangu kuingia madarakani kwa Nelson Mandela pamoja na chama chake cha Afikan National Congress mwaka 1994.

Lakini hata hivyo biashara nyingi kubwa kubwa katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita zimekuwa zikiwahusisha miamba wanaohusiana na chama cha ANC na kusababisha hasira miongoni mwa wakosoaji ambao wanasema sera hiyo inataka kuunda kikundi cha wafanyibiashara matajiri tu nchini humo.

Wakosoaji hao wameitolea wito serikali ya Afrika Kusini kurekebisha muongozo wa sera hiyo ili kuhakikisha faida yake inagawanywa kwa usawa zaidi kote nchini na wachambuzi wanahisi kuna mkondo wa kuelekea maendeleo katika lengo la kufikiwa kwa hatua hiyo.

Wafanya biashara wadogo wadogo wa kiafrika kama Bibi Gloria Serobe na kikundi chake cha kupigania nafasi ya wanawake upande huo, ni miongoni mwa walionufaika na mpango wa dola bilioni 1 na milioni 6.

Maafisa wa serikali wanasema mamia ya makampuni madogo madogo sasa yameanza kufaidika kutokana kandarasi kwa mfano za usafishaji na ukarabati au kutokana na mikataba ya utengenezaji sare, kwa kuwa makampuni makubwa yana hamu ya kuonyesha kuwa kuna mabadiliko.

Boniswa Seakanela ambaye ni meneja wa Stoo mjini Soweto anakubaliana na hayo akisema " Tunahitaji kuona mkate ukigawanywa ipasavyo".

Wakosoaji wanasema muongozo wa kuwapa nafasi waafrika katika masuala ya kibiashara nchini Afrika kusini, hauna budi kutekelezwa na kuheshimiwa, lakini kuna wanaohoji kwamba serikali imeshindwa kuwajibika ipasavyo katika suala la usambazaji utajiri chini ya mpango huo wa BEE, ili uweze kumfikia hata mtu wa kawaida barabarani, na sio kuzunguka tu miongoni mwa watu wa wale wa kikundi fulani tu .

Wanatoa wito kwa hivyo, kuweko na muongozo katika kila sekta ili kuepusha makosa ya hapo kabla. Sekta nyingi zimefuata mfano wa sekta ya maadini, ambayo ilianza kufuata muongozo huo miaka miwili iliopita, na ambao umekua ni mfano wa kuigwa katika suala la kugawanya utajiri kwa waafrika katika hali ya usawa na sambamba na hayo kuboresha ujuzi wao makazini.

Tatizo jengine kubwa kwa watu wa kawaida ni ukosefu wa fedha za kujiendeleza wenyewe. Kwa upande huo muuzaji na mmiliki wa duka moja mjini Soweto kwa jina la Kevin Tshepo anasema"tatizo ni kwamba watu hawana fedha za kukuza biashara zao, watu wanasikia tu ju ya haja ya kupewa nafasi za kujiendeleza kupitia redioni, na kujiuiliza ni waafrika gani wanaozungumzwa na ambao wameweza au wanaweza kujitajirisha kwa njia ya kujitegemea wao wenyewe ?"

Kwa mujibu wa mkakati wa serikali,, sekta ya huduma za fedha na viwanda ina waraka unaoahidi kwamba 25 asili mia ya sekta hiyo iwe inamilikiwa na waafrika ifikapo 2010, ambapo 10 asili mia uwe ni umilikaji wa moja kwa moja na sio kuwa na hisa. Sehemu iliobakia ya 15 asili mia ndiyo iwe kwa njia za hisa za moja kwa moja.