Afrika Kusini yatafakari kuwapa vibali vya muda Wazimbabwe
29 Agosti 2007Waziri wa mambo ya ndani wa Afrika Kusini, Nosiviwe Mapisa- Nqakula, amenukuliwa akisema serikali imekubali kutafuta njia mpya ya kukabiliana na wakimbizi wasio halali wanaovuka mpaka na kuingia Afrika Kusini kutoka eneo la kaskazini mwa Zimbabwe kila siku. Huku serikali ikiendelea kushikilia msimamo wake wa kutowapa ukimbizi, waziri Mapisa Nqakula amesema vibali vya muda vinaweza kuwa njia ya kuwawezesha kuishi nchini Afrika Kusini kihalali.
´Njia moja ni kuwapa vibali vya muda, ´alisema Bi Mapisa wakati alipokuwa akilihutubia bunge mjini Cape Town lakini akasema hangeweza kutoa maelezo zaidi kuhusu pendekezo hilo kwa sababu bado linahitaji kujadiliwa na baraza la mawaziri. Aidha waziri Mapisa alisema kuwapa vibali vya muda Wazimbabwe kutawawezesha kufanya kazi nchini Afrika Kusini na wao kama viongozi wa serikali wana jukumu la kuwapa changamoto Wazimbabwe waitumie fursa hiyo.
Wazimbabwe wengi wanaokimbilia Afrika Kusini hupendelea kufanya kazi ili wajipatie fedha za kuweza kuzisaidia familia zao. Baadhi yao huitembelea Zimbabwe mara moja kila mwezi. Waziri Mapisa Nqakula amesema ni kupoteza fedha kuwarudisha makwao Wazimbabwe kila wiki kwa kuwa wengi kati ya wale wanaorudishwa hurejea Afrika Kusini siku chache baadaye.
Waziri huyo amesisitiza kwamba serikali haitajenga kambi mpya za wakimbizi karibu na mipakani kukabiliana na wimbi la wahamiaji kutoka Zimbabwe, akisema kwa kufanya hivyo Wazimbabwe wengi watavuka mpaka kuja kujipatia mlo na baadaye kurejea Zimbabwe. Zimbabwe inakabiliwa na mfumuko wa bei wa zaidi ya asilimia 7,600, huku asilimia 80 ya Wazimbabwe wakiwa hawana ajira. Zaidi ya Wazimbabwe milioni tatu wameikimbia hali ngumu ya kiuchumi, wengi wao wakihamia Afrika Kusini.
Wakati haya yakiarifiwa, gazeti linalomilikiwa na serikali ya Zimbabwe, The Herald, limeilaumu Australia kwa kujaribu kumuondoa madarakani rais Robert Mugabe na kuitaka serikali ya mjini Harare iwafukuze wanadiplomasia wa Australia walio nchini humo. Australia, Marekani na Uingereza zimekuwa msitari wa mbele kumkosoa rais Mugabe, kuiwekea vikwazo serikali yake na kutaka uchaguzi huru na waki ufanyike nchini humo.
Gazeti la The Herald limeishutumu Australia kwa kupanga kumuondoa rais Mugabe kama sehemu ya njama ya Uingereza ya ubaguzi wa rangi katika juhudi za kukiweka madarakani chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe, Movement for Democratic Change, MDC. Mhariri wa gazeti la Herald alisema uhusiano wa kidiplomasia baina ya Australia na Zimbabwe hauwezi kuvumilika tena wakati huu wa utawala wa waziri mkuu John Howard.
Chaguo pekee lililosalia kwa Zimbabwe ni kufunga ubalozi wake mjini Sydney na iamuru ubalozi wa Australia mjini Harare ufunge virago vyake na uondoke. Gazeti la Herald lilisema hakuna hasara yoyote itakayopata Zimbabwe kwa kufunga ubalozi wake mjini Sydney na kuwaamuru maafisa wa ubalozi wa Australia mjini Harare, wanaotumwa kuhudumu kwa miaka mitatu, waondoke.
Mugabe, mwenye umri wa miaka 83, ameongoza tangu mwaka 1980 baada ya Zimbabwe kutawaliwa na Uingereza kwa miongo kadhaa. Wakosoaji wanamlaumu Mugabe kwa kuisukuma Zimbabwe katika hali ngumu ya kiuchumi kwa kuanzisha sera kama vile kuyachukua mashamba yaliyokuwa yakimilikiwa na wazungu na kuwagawia Wazimbabwe asili.
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Australia, Alexander Downer, na kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe, Morgan Tsvangirai, wamezitolea mwito nchi barani Afrika, hususan Afrika Kusini, zimshinikize rais Mugabe na kumshawishi afanye uchaguzi huru na wa haki. Bwana Tsvangirai anatarajiwa kufanya mazungumzo na waziri mkuu wa Australia, John Howard, baadaye wiki hii.