1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika kusini yawafukuza Wazimbabwe

Jane Nyingi8 Januari 2009

Afrika Kusini imetakiwa kulegeza sheria zake kuhusu idadi ya wahamiaji kutoka Zimbabwe inayowaruhusu kuishi nchini humo.

https://p.dw.com/p/GUeW

Shirika la kimataifa la kupigania haki za binadamu, Human Rights Watch, limeitaka afrika kusini isimamishe mara moja shughuli ya kuwafukuza Wazimbabwe nchini humo na kuwapa vibali vya muda kuishi na kufanya kazi Afrika Kusini.

Ili kuzuia kufukuzwa nchini Afrika Kusini, Wazimbabwe wamelazimika kuomba hifadhi nchini humo, na hivyo kuifanya Afrika Kusini kukabiliwa na mzigo mkubwa wa kuhudumia idadi ya wakimbizi. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, idadi ya Wazimbabwe waliomba hifadhi katika muda wa miezi mitano tangu mwaka jana katika mji ulio mpakani wa Musina ni kati ya elfu 20 na 30.

Idadi hii ni zaidi ya nusu ya raia kutoka mataifa mengine ambao wanaomba hifadhi nchini humo.Hadi sasa afisi za uhamiaji nchini humo hazijaweza kutatua zaidi ya kesi elfu 100. Kufurika kwa Wazimbabwe nchini Afrika Kusini kunawafanya wakimbizi wengine walioko nchini Afrika kusini kukabiliwa na tatizo la maombi yao kukataliwa.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na shirika la Human Rights Watch, Wazimbabwe walioko nchini Afrika Kusini wamekuwa wakipitia mateso chungu mzima kwa kuchukuliwa na wenyeji kuwa ni maadui. Afisi za uhamiaji nchini Afrika Kusini pia zimekuwa zikipuuza maombi ya kupatiwa hifadhi kutoka kwa Wazimbabwe na hata wakati mwingine kuwazuia kutoa malalamishi ya aina yeyote.

Ripoti hiyo ya shirika la Human Rights Watch inaendelea kuonyesha jinsi zaidi ya Wazimbabwe elfu 250 wamekuwa wakifuzwa nchini Afrika kusini kinyume cha sheria kila mwa mwaka, hali inayokiuka sheria za kimataifa za wakimbizi.

Shirika la kimataifa la Human Rights Watch limekuwa likifuatilia kwa kina na kuandika taarifa kuhusu visa vya kukiukwa haki za kibindamu nchini Zimbabwe, kama vile ghasia za kisiasa na kutiwa mbaroni bila sababu yeyote wanaokipinga chama tawala nchini Humo, ZANU-PF. Hata kwa mujibu wa Issac Khomo mwandishi habari nchini Afrika Kusini wazimbabwe wamekuwa wakihusika katika visa vya uhalifu afrika kusini.

Katika ripoti ya mwezi November mwaka jana,iliyopewa jina “Our hands are tied' yaani mikono yetu imefungwa, ilieleza njisi utaratibu wa sheria unavyokiukwa nchini Zimbabwe na kuwafanya majaji,mahakimu na kikosi cha polisi kuegemea upande wa chama tawala cha rais Robert Mugabe.

Zimbabwe inakabiliwa na mzozo wa kiutu, huku mfumo mzima wa afya ukiporomoka katika muda wa miezi minne iliyopita.Hospitali kuu za umma mjini harare,mji mkuu wa Zimbabwe, zimefungwa na kuna upungufu wa dawa na wahudumu wa mahospitali kote nchini Zimbabwe. Vifo kutokana na kuzuka kwa ugonjwa wa kipindupindu katika miji mikuu nchini Zimbabwe na miji mingine midogo vimeendelea kuripotiwa, huku kukiwepo upungufu wa maji safi ya kutumiwa na bindamu.

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la afya ulimwenguni WHO,kuanzia mwanzo wa mwaka huu Wazimbabwe 1732 wamefariki kutokana na ugonjwa wa kipindupindu na zaidi ya elfu 34 wameambukizwa Ugonjwa huo unatarajiwa kuzuka upya msimu wa mvua unapoingia mwezi ujao, hali amabyo husababisha mafuriko.Shirika la UNICEF limekadiria kuwa visa vya ugonjwa huo huenda vikafikia elfu 60 au zaidi katika muda wa miezi michache.