1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika kusini

Nyanza, Halima22 Mei 2008

Siku moja baada ya Rais Thabo Mbeki wa Afrika kusini, kuidhinisha jeshi kusaidia kudhibiti wimbi la ghasia dhidi ya wahamiaji wa Kiafrika nchini humo, ambapo mpaka sasa watu 24 wameuawa, ghasia hizo bado zinaendelea.

https://p.dw.com/p/E4FE
Mhamiaji wa Kiafrika nchini Afrika kusini, akiwa hoi baadaya kupigwa na magenge ya watu nchini humo, wasiotaka wageni hao, kwa madai ya kuwachukulia ajira zao.Picha: AP

Wakati Jeshi la Afrika kusini likijianda kuingia katika vitongoji nchini humo, kuweza kusaidia kumaliza mashambulizi ya chuki yanayofanywa na wenyeji dhidi ya wahamiaji wa Kiafrika nchini humo, yaliyosababisha watu 42 kuuawa, baada ya kutolewa idhini na Rais Thabo Mbeki, Makamu mwenyekiti wa chama tawala nchini humo cha Afrika  National Congres ANC, Kgalema Motlanthe amekosoa polisi kutokana na kuchelewa kwao kushughulikia tatizo hilo.

Zaidi ya wafanyakazi wahamiaji wapatao elfu 15 na familia zao wamekimbilia katika kambi za wakimbizi, baada ya siku 11 za mashambulizi hayo dhidi ya wahamiaji wa Kiafrika, yanayofanywa na magenge ya watu wenye silaha kwa kudai kuwa wageni hao wanachukua kazi zao na kusababisha vitendo vya uhalifu.

Watu kadhaa wamechomwa moto hadi kufa na wengine kuteswa kutokana na ghasia hizo.

Ghasia hizo mpaka sasa zimesababisha raia wa Msumbiji wapatao elfu 9, wanaoishi nchini humo, kuondoka tangu mashambulizi hayo dhidi ya wahamiaji wa Kiafrika yalipoanza Mei 11, katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa Johanesburg.

Raia hao wa Msumbiji wanafikiriwa kuwa ni wa pili kwa wingi nchini humo, baada ya wahamiaji kutoka Zimbabwe ambao ndio wanaoongoza.

Wahamiaji kutoka nchi nyingine za Afrika, ikiwemo Zimbabwe na Malawi wameonekana pia wakiondoka nchini humo kwa kutumia usafiri wa mabasi, kutokana na ghasia hizo, ambapo katika siku za hivi karibuni zimesababisha watu elfi 16 kukosa makazi na wengine takriban 400 kukamatwa.

Ingawa ghasia hizo zijnazofanywa na wenyeji dhidi ya wahamiaji wa Kiafrika zinatokea sana katika maeneo ya mji wa Johannesburg, lakini mashambulizi hayo ya chuki yameripotiwa kutokea pia katika mji wa Durban na katika jimbo la mashariki la Mpumalanga.

Polisi nchini humo wamearifu kuwa raia mmoja wa Msumbiji aliuawa na mabasi wawili kuchomwa moto jana usiku katika eneo moja la kitongoji hicho, na kwamba kundi la wahamiaji kutoka nchi za Somalia, Msumbiji na Zimabwe wamepata hifadhi ya ukimbizi katika kituo kimoja cha polisi jimboni humo.

Jana Rais Thabo Mbeki aliridhia ombi la polisi la kutaka kuungwa mkono na jeshi katika kuzima ghasia hiyo, lakini bado haijafahamika ni lini ni lini jeshi hilo litasambazwa.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Fedha wa nchi hiyo Trevor Manuel, amesema ufumbuzi wa tatizo hilo ni kubadili maisha ya kila siku ya watu na kwamba kuitwa kwa jeshi si kupata suluhu ya suaka hilo.

Amesisitizia mahitaji ya kupunguza ukosefu wa ajira miongoni mwa raia wa nchi hiyo, ambapo ni asilimia 23 ya watu, lakini vyama vya wafanyakazi nchini humo vinakadiria kuwa karibu asilimia 40.

Wakati baadhi ya raia wa Afrika kusini wakitenda hayo, wengine wamekuwa yakiwasononesha.

Matukio hayo ya ghasia zinazosababisha mauaji, zimekuwa zikikumbushia enzi mbaya za ubaguzi wa rangi nchini humo, halia mabayo pia imefanya mashirika ya kiutu kukusanya misaada kwa ajili ya kuwasaidia waliokumbwa na tatizo hilo.

Vyama vya Wafanyakazi, wanasiasa na viongozi wa jamii mbalimbali wamekuwa wakilaani ghasia hizo.

Baadhi ya Waafrika kusini wamekuwa wakiwaruhusu wafanyakazi wao wa kigeni kutoka nchi nyingine za Afrika, kulala majumbani mwao ili kuepuka na ghasia hizo.

Vikundi vya misaada vimekuwa katika harakati kuweza kuwasaidia takriban watu elfu 16, ambao kwa sasa hawana makazi kutokana na ghasia hizo dhidi ya wahamiaji wa Kiafrika.

Mwenyekiti wa kikundi kimoja kinachoshughulikia masuala hayo ya kiutu Imtiaz Sooliman anasema watu nchini humo wanajisikia aibu na yanayotokea, na kuelezea hali mbaya iliyopo kwa watu hao, hivyo kuhitaji msaada.

Zaidi ya dola 131,000 zimekusanywa kwa jili ya kusaidia watu hao.