Afrika ya Kati yaidhinisha rasimu ya katiba mpya
8 Agosti 2023Jamhuri ya Afrika ya Kati, mojawapo ya nchi masikini zaidi na zenye migogoro ulimwenguni, na ambayo imezingirwa na mipaka ya nchi kavu, imekumbwa na machafuko na mtafaruku wa kisiasa, kwa kipindi kirefu cha historia yake baada ya kupata uhuru kutoka kwa Ufaransa mwaka wa 1960.
Soma pia: Kura zahisabiwa Jamhuri ya Afrika ya Kati
Wapinzani wa Rais Touadera wanasema anataka kuwa "rais wa maisha” – chini ya ulinzi unaoendelea kuonekana wazi wa kundi la mamluki wa kibinafsi wa Urusi la Wagner, ambalo lilipeleka askari wake nchini humo kwa mara ya kwanza katika mwaka wa 2018.
Rais wa tume ya kitaifa ya uchaguzi Mathias Morouba amesema Idadi ya walioshiriki kura hiyo ya maoni ya Julai 30 ilikuwa asilimia 61.10. "Kwa kuzingatia yaliyosemwa, Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Afrika ya Kati iliyowasilishwa kwenye kura ya maoni, ilipata kura 1,064,729, ambazo ni sawa na asilimia 95.27. Kwa mujibu wa Ibara ya 3, uamuzi huu, ambao unaanza kutumika tangu tarehe ya kutiwa saini, utachapishwa popote inapobidi."
Matokeo lazima yaidhinishwe na mahakama ya kikatiba, ambayo inatarajiwa kuchapisha matokeo rasmi ya zoezi hilo Agosti 27.
Katiba hiyo mpya itarefusha muhula wa rais kutoka miaka mitano hadi saba na kuondoa ukomo wa kuongoza kwa mihula miwili. Hakuna vizingiti vya kumzuia Touadera mwenye umri wa miaka 66 kugombea kwa muhula wa tatu katika mwaka wa 2025. Kama atachaguliwa, huenda akasalia madarakani kwa miaka 16.
Soma pia: Bangui wapiga kura kubadilisha katiba
Upinzani wasusia
Kura hiyo ilisusiwa na vyama vikuu vya upinzani na mashirika ya kiraia, pamoja na makundi ya waasi. Upinzani ulilalamika kuhusu ukosefu wa daftari la wpaiga kura lililopitiwa upya na kuboreshwa na kusema taasisi zilizopewa dhamana ya kuhakikisha uchaguzi wa huru na haki haziko huru.
Shirika la Kimataifa la Haki za Binaadamu – Human Rights Watch linasema maafisa wa serikali wamejaribu kuwatishia wapinzani wa kura ya maoni, na serikali pia ikapiga marufuku mkutano wa hadhara wa upinzani katika mji mkuu Bangui katika jaribio la kufunika uhasama kwa kura hiyo.
Crepin Mboli-Goumba, mratibu wa muungano wa upinzani wa BRDC anasema ni kichekesho, kwa sababu watu hawakwenda kupiga kura na hiyo haionyeshi mapenzi ya watu wa Afrika ya Kati.
Touadera alichaguliwa kwa mara ya kwanza katika mwaka wa 2016 wakati nchi hiyo, kwa msaada wa Ufaransa na Umoja wa Mataifa iliibuka kutoka vita vya wenywe kwa wenyewe ambavyo vilifanyika kwa misingi ya kidini kufuatia mapinduzi. Alishinda muhula wa pili wa miaka mitano katika mwaka wa 2020, uchaguzi uliovurugwa na mashambulizi kadhaa ya makundi ya waasi. Pia alikabiliwa na tuhuma za udanganyifu.
AFP