Ahadi za kushusha kodi ni kampeni tupu za uchaguzi ujao ?
22 Aprili 2009Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo yamechambua mada mbali mbali-nyingi zikiwa za ndani kama vile sadaka inazoahidi kutoa chama cha Social Democratic party (SPD) kwa wapiga kura katika uchaguzi ujao,msukosuko wa uchumi nchini Ujerumani na ripoti juu ya data au taarifa zinazokusanywa za wananchi.
Gazeti la Hannoversche Allgemeine Zeitung kuhusu ahadi za chama cha SPDlaandika:
"Kutoa ahadi zisizotekelezeka katika mfumo mpya wa kodi, si jambo la kutiwa maanani.Kupiga debe katika kampeni za uchaguzi na kutekeleza ahadi kivitendo kwa jicho la kukaribia tarehe ya uchaguzi ujao ni peya 2 za tofauti za viatu.Ikiwa navyo vyama vya CDU/CSU karibuni vitatangaza kupunguza kodi,yapasa pia kuwa na hadhari navyo."
Likizungumzia msukosuko wa sasa wa kiuchumi, gazeti la Badische Neueste Nachrichten laandika:
"Makampuni mengi ya Ujerumani yamekumbwa n a msukosuko.Hayajipatii kandarasi za kutosha.Ni sehemu ndogo tu ya makampuni hali haiko hivyo.Nayo ni Taasisi za kiuchumi.Tabia yao kila kwa mara kubashiri mambo yasiodhihirika kuwa kweli haikubadilika na hazipepesuki na msukosuko wa sasa wa kiuchumi........Taasisi hizi zinapokuja kuishauri serikali ya Ujerumani nini la kufanya ,huwa zimejiweka katika daraja ya watakatifu."
Ama gazeti la Stuttgarter Nachrichten laandika:
"Wanasiasa hawamudu kila mara kutoa mabilioni ya Euro kutengeneza pale mameneja wa viwanda waliko haribu.Mwavuli wa kuwakinga unabidi haraka kufungwa.Ushawishi wa serikali haraka uwekewe mpaka.
Tangu kuzuka kila sekta msukosuko,miradi ya kuwasaidia wanyonge imesimama............katika kipindi kijacho cha utawala, serikali inayokuja inabidi kufanya mageuzi yasiowapendeza watu.Kasoro ziliopo wakati huu katika hazina ya mfuko wa wasio na kazi na ya bima ya afya inaanza kutisha."
Gazeti la Frankfurter Rundfschau linazungumzia rai gani ya kufuatwa na serikali ya Ujerumani kuyasafisha mabenki na hisa chafu katika mabenki hayo ?Lauliza:
"Ikiwa serikali iyasafishe mabenki na uchafu wa hisa za aina hiyo ,swali ni kwa gharama gani ? Ikiweka thamani ya chini, mabenki yatafilisika hii leo.Thamani hiyo ikipandishwa mno, mlipakodi atabidi kugharimia hasara zake.Na hii ndio hasa iliopanga kufanya wizara ya fedha.
Serikali inapanga kuteua halmashauri ya mabingwa kutathmini thamani ya mikopo inayoregarega.Furaha ilioje.Hatari iliopo ni kuwa, mabingwa hao waweza kuweka thamani kubwa mno.Mabenki yatawatupia hapo walipakodo mzigo wa kulipa gharama ya hisa hizo,kwavile, yanaelewa sehemu kubwa ya fedha hizo hayatazipata tena.
Muandishi: Ramadhan Ali
Mhariri : M.Abdul-Rahman / DPA