ANC kumchagua kiongozi wao.
18 Desemba 2007Polokwane, Afrika kusini.
Wajumbe wa chama tawala nchini Afrika kusini wameanza zoezi la kumchagua kiongozi wao leo Jumanne wakati ishara zote zikionyesha kushindwa kwa rais Thabo Mbeki dhidi ya hasimu wake mkubwa kisiasa Jacob Zuma.
Gazeti la Star limeandika katika ukurasa wake wa mbele leo kuwa , jukwaa liko tayari kwa ajili ya ushindi wa Zuma. Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 65, alikuwa wa kwanza miongoni mwa wajumbe 3,900 kupiga kura katika ukumbi wa mikutano wa chuo kikuu cha Limpopo.
Zuma , ambaye alipowasili katika ukumbi huo alishangiliwa sana na wajumbe , waliokuwa katika mstari wa kupiga kura , alionekana mwenye kujiamini na kuwapungia wafuasi wake kabla ya kuingia katika chumba cha kupigia kura katika eneo la chuo hicho.