ANC kumchagua rais wa chama.
18 Desemba 2007Polokwane, Afrika kusini. Wajumbe wa chama tawala nchini Afrika kusini cha ANC wamepiga kura leo kumchagua rais mpya wa chama hicho katika uchaguzi wenye mvutano mkubwa ambapo makamu wa rais wa chama hicho Jacob Zuma anatarajiwa kushinda. Wafuasi wa rais wa sasa Thabo Mbeki wanamatumaini kupata kuungwa mkono kwa dakika za mwisho kwa kiongozi wao. Mbeki alimfuta kazi Zuma wakati akiwa makamu wa rais mwaka 2005 baada ya kuhusishwa katika kashfa ya ufisadi. Alituhumiwa na baadaye kushtakiwa lakini aliachiwa huru kwa makosa ya ubakaji. Iwapo atachaguliwa kuwa rais wa ANC, inawezekana akawa rais wa nchi hiyo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2009 kutoka na umaarufu mkubwa miongoni mwa Waafrika wa nchi hiyo waliowengi.