ANC yaijadili changamoto inayoikabili.
16 Oktoba 2008Chama tawala nchini Afrika kusini African National Congress-ANC, kimeungama kwamba kundi linalotaka kujitenga na kuunda chama kipya linakipa "changamoto kubwa ya kisiasa" na hivyo kimekula kiapo kuchukua hatua kali dhidi ya mwanachama yeyote atakayejiunga na chama kipya.
Baraza kuu la taifa la ANC limearifu kwamba litaanza zoezi la kujadili nidhamu ya wanasiasa wa ngazi ya juu waliotangaza mipango ya kujie´ngua. Akizungumza na waandishi habari leo mjini Johannesburg, Katibu mkuu wa ANC Gwede Mantashe alisema baraza hilo kuu la taifa, lina jukumu la kuchukua hataua dhidi ya watakaokiuka misingi na kwenda kinyume na utekelezaji au nidhamu ya chama .
Akaongeza kwamba wanaliangalia tangazo la baadhi ya wanachama wa ANC kutaka kuunda chama kipya kuwa ni la upinzani dhidi ya ANC na kwamba baraza kuu la taifa linakubaliana hali hiyo lazima ikabiliwe kisiasa. Hata hivyo alieleza kwamba wanachokiona hivi sasa si mgawanyiko bali ni upinzani wa watu wachache. Bw Mantashe akaeleza kuwa,"Hatuwezi kuzungumzia mgawanyiko kwa sasa, lakini tunachokiona ni wapinzani wachache wanaoozusha masuala yao hadharani na kujaribu kushajiisha mtengano."
Awali viongozi wa chama hicho tawala nchini Afrika, walipuuza kitisho cha kuundwa chama kipya na wale wenye azma ya kujitoa, wakisema hakuna anayeweza kushindana na ANC, chama kikongwe kabisa cha ukombozi barani Afrika na ambacho kiko madarakani tangu kumalizika kwa utawala wa kibaguzi.
Waziri wa zamani wa ulinzi Mosiuoa Lekota na vigogo wengine katika ANC wanapanga kuitisha mkutano mkuu wa kitaifa tarehe 2 mwezi ujao wa Novemba, ambapo inatarajiwa awatatangaza kuunda chama kipya cha kisiasa kushindana na ANC katika uchaguzi mkuu ujao Aprili mwakani.
Lekota alisimamishwa uwanachama wa ANC Jumatatu na hatua nyengine kali inayoweza kufuata ni kufukuzwa chamani. Katika tukio la kushangaza jana waziri mkuu wa zamani wa mkoa tajiri kabisa nchini humo wa Gauteng Mbhaziwa shilowa alitangaza kujitoa ANC kujiunga na Bw Lekota.
Mbhaziwa alijuzulu uwaziri mkuu kupinga kulazimishwa kujiuzulu Thabo Mbeki kama rais wa tarehe 20 mwezi uliopita wa Septemba.Katibu mkuu Mantashe, alisema "yeyote atakayedhubutu kuwashawishi wanachama wa ANC kujiunga na chama kipya atachukuliwa hatua za kinidhamu, kwa sababu hatuwezi kuwaruhusu watu wajaribu kuiangamiza ANC." Bw Mantashe akawaita hao kuwa watu waliolewa madaraka akisema," Watu waliolewa madaraka wanapoondolewa madarakani watafanya lolote lile kwa sababu wameshalewa madaraka."
Maafisa wa ANC kwa upande mwengine awamekanusha kwamba wanapanga kuitisha uchaguzi mkuu wa mapema, katika kile kinachoonekana ni jaribio la kutaka kuzuwia ushawishi wa chama kipya pindi kitaundwa.
Lekota na waasi wengine chamani wanaoungana naye-wote ni wafuasi wa rais wa zamani Thabo Mbeki, ambaye alilazimishwa kujiuzulu kama rais wa taifa . Hadi sasa Mbeki binafsi hakutamka lolote juu ya uwezekano wa mgawanyuiko ndani ya ANC. Lakini mgawanyiko huo ni jambo ambalo limekua likizungumzwa tangu kumalizika mkutano mkuu miezi michache iliopita, pale Bw Jacob Zuma alipomshinda Mbeki katika kinyanganyiro cha Uongozi wa ANC.