1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Arab League waikemea Marekani lakini washindwa kuigomea

10 Desemba 2017

Mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wametaka kufutwa kwa uamuzi wa Rais Donald Trump kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel, lakini wameshindwa kuichukulia hatua Marekani.

https://p.dw.com/p/2p5xc
Ägypten Minister der Arabischen Liga tagen in Kairo
Picha: Reuters/M. Abd El Ghany

Mawaziri hao waliokutana mjini Cairo, Misri, katika mkutano wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu wameuita uamuzi huo wa Trump kuwa ni hatua ya hatari sana ambayo inaiweka serikali ya Marekani kwenye upande mmoja na "ukaliaji" na uvunjaji wa sheria za kimataifa.

Katika azimio lao lililojaa maneno makali lakini lenye uchache wa hatua za kuchukuliwa, mawaziri hao pia walilitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupitisha azimio la kuulaani uamuzi wa Trump, ingawa walikiri kuwa kuna uwezekano mkubwa wa azimio hilo kupigiwa kura ya turufu na Marekani. 

Hata hivyo, Waziri wa Nje wa Palestina, Riyad Al-Maliki, alisema kuwa endapo Marekani italipigia kura ya turufu azimio hilo, mataifa ya Kiarabu yatasaka azimio jengine kupitia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. 

Azimio la kurasa tatu lililotolewa baada ya mkutano huo wa dharura, ambao ulianza usiku wa Jumamosi (9 Disemba), halikujumuisha hatua za kuiadhibu Marekani, kama vile wito wa kususia bidhaa za Kimarekani au kukata mahusiano ya kibalozi au kushusha hadhi mahusiano hayo.

Azimio jepesi

Kinyume na ilivyotarajiwa na wengi, azimio la Umoja wa Nchi za Kiarabu lilikuwa jepesi zaidi kulinganisha na hasira zinazooneshwa na Wapalestina katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, ambamo mumeshuhudiwa maandamano ya ghadhabu na ghasia dhidi ya uamuzi huo wa Trump.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Ahmed Aboul Gheith.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Ahmed Aboul Gheith.Picha: Reuters/M. Abd El Ghany

"Tumechukuwa uamuzi wa kisiasa usiokusudia kuakisi kinachoendelea mitaani. Kazi ya kisiasa ni kazi ya dhamana," alisema mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiarabu, Ahmed Aboul-Gheith. "Jerusalem imekaliwa kwa miaka 50. Hivi ni vita vinavyopanuka, mapambano yatazidi," aliwaambia waandishi wa habari.

Tamko hilo lilisema kuwa mawaziri hao watakutana tena ndani ya kipindi cha mwezi mmoja na kuonesha uwezekano wa kufanyika kwa mkutano wa kilele wa dharura nchini Jordan kujadili suala la Jerusalem.

Tangazo la Trump la hapo Desemba 6 na dhamira yake ya kuuhamishia ubalozi wa Marekani kwenye mji wa Jerusalem ulizua lawama kote ulimwenguni, hata kutoka kwa washirika wa karibu, wakisema kuwa ameutiribua mzozo pasina sababu.

Hadhi ya Jerusalem ni kiini cha mgogoro kati ya Israel na Palestina na hatua ya Trump ilichukuliwa kwa kiasi kikubwa kuwa ni kuonesha kujiegemeza upande wa Israel. Katika siku za nyuma, hata ugomvi mdogo kuhusiana na hadhi ya Jerusalem ama maeneo yake matukufu umekuwa ukizuwa machafuko makubwa na umwagaji damu.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/AFP
Mhariri: Grace Patricia Kabogo