Ardhi ya Ahadi – Hadithi ya Uhamiaji wa Waafrika barani Ulaya
12 Agosti 2013Ni kitu gani kinachowasukuma vijana wengi barani Afrika kutafuta maisha mapya Ulaya? Wanafika vipi huko? Na je, ndoto zao hutimia punde wanapofika Ulaya? Mchezo huu wa Noa Bongo Jenga Maisha Yako wenye sehemu 15, unaangazia maisha halisi ya wahamiaji kutoka Afrika.
Unawafuatilia kuanzia wakati wanapoamua kuondoka makwao Afrika, kuangalia njia mbalimbali za usafiri wanazotumia kufika Ulaya na kuangazia wanayoyapitia mara wanapowasili barani humo.
Huko Afrika ya Kaskazini tunakutana na Farahani na Sule. Marafiki hawa wawili hawana ajira na wana kitu kimoja tu akilini mwao: Ulaya! Wana dhamira kubwa ya kusafiri kwenda Ulaya kiasi kwamba ingawa hawana viza za kusafiria na safari ni ya hatari, wako tayari kuhatarisha maisha yao. Mara tu anapowasili Ulaya, Sule anatambua kuwa maisha huko sivyo kabisa kama alivyotarajia…
Katika kijiji kimoja kusini mwa jangwa la Sahara, Linda, msichana mwenye umri wa miaka 20, analazimika kumuaga mchumba wake, Chivasi, kwa sababu wazazi wake wameamua kwamba anatakiwa kuendelea na masomo yake Ulaya. Wakati Linda anapowasili Ulaya, anakutana na Florence, mwanamke mwingine kutoka Afrika.
Mwanzoni Florence anaonekana akimsaidia sana Linda, lakini baadaye inabainika kuwa si rafiki wa dhati... Linda analazimika kukabiliana na changamoto nyingi kama vile kutafuta viza, kuondokana na mshituko wa kitamaduni, fikra nyingi za kutamani nyumbani na kuukubali ukweli kwamba amewaacha marafiki zake na familia yake Afrika.
Hadithi za Sule, Farahani, Linda na Chivasi zinagusia baadhi ya sababu kwa nini wahamiaji wengi wa Afrika huondoka barani mwao. Zinaangazia pia matatizo wanayokumbana nayo wakiwa safarini kuelekea Ulaya na wakati wanapowasili.
Mchezo huu kwa jina la “Ardhi ya Ahadi” ni sehemu ya mradi wa vipindi vinavyotayarishwa na Deutsche Welle kuhusu “Uhamiaji Barani Ulaya” (Angalia kwenye tovuti ya kiingereza).
Noa Bongo Jenga Maisha Yako ni vipindi vinavyotayarishwa na Deutsche Welle na vinasikika katika lugha sita ikiwa ni pamoja na Kiingereza, Kiswahili, Kifaransa, Kihausa, Kireno na Kiamhara.