Arsenal yataka kuonyesha maajabu
13 Machi 2013Wakati timu hizo zitakapokutana tena leo jioni(13.03.2013) katika mchezo wa mwisho wa kuamua nani ataingia katika robo fainali. Hii ni kwa mujibu wa kocha wa timu hiyo Aserne Wenger. Mchezo mwingine ni kati ya Porto ya Ureno dhidi ya Malaga ya Uhispania.
Arsenal inaonekana kuwa timu ya tatu katika historia ya mashindano hayo , kufungwa nyumbani katika duru ya mtoano lakini hatimaye kuweza kushinda ugenini na kusonga mbele.
Wachezaji kadha wa Arsenal hata hivyo hawatakuwamo katika kikosi hicho , nao ni pamoja na Jack Wilshere, Lukas Podolski na Bacary Sagna, na hali hii imeufanya mzigo mzito unaokabili timu hiyo mbele ya Bayern kuwa mkubwa zaidi , lakini Wenger amesema timu yake iko tayari kufanya maajabu makubwa.
Mtaduwaa
"Ni matumaini yangu kuwa tutamshangaza kila mtu leo jioni," amesema Wenger huku akitabasamu wakati akizungumza na waandishi habari. "Ndio tunamajeruhi lakini tumekuja hapa na kikosi kizuri ambayo ina motisha.
"Kitu muhimu ni kuingia katika mchezo huu kwa kuweka mbinyo haraka na kupata goli la mapema. Imani yetu haijaweza kujaribiwa kama itakavyokuwa jioni ya leo, amesema kocha huyo raia wa Ufaransa.
Wenger ambaye amemuacha nyumbani London mlinda mlango namba moja wa timu hiyo Wojciech Szczesny akisema mchezaji huyo amechoka kiakili baada ya msimu mrefu , amesema kuwa timu yake itahitaji kupata uwiano sahihi baina ya nia halisi na uhuru uwanjani kutokana na matokeo ya awali katika mchezo wa kwanza.
"Ni hali ngumu, ndio lakini kwamba haiwezekani , hapana, amedokeza Wenger.
Kocha wa Bayern Munich Jupp Heynckes amewaonya wachezaji wake watarajie kisichotarajiwa kutoka kwa kikosi cha Wenger.
Henckes awatahadharisha Bayern
"Tunapaswa kuwa waangalifu , hata kama tumeshinda mchezo wa kwanza kwa mabao 3-1.
"Mafanikio yamekuja kwa Arsenal wakati Arsene alipowasili katika timu hiyo.
"Kwa muda wa miaka mingi walicheza soka nzuri sana nchini Uingereza, kama sio kila mara timu iliyopata mafanikio makubwa.
Wakati huo huo Sir Bobby Charlton mchezaji wa zamani wa kikosi cha Uingereza kilichonyakua ubingwa wa dunia kwa mara ya kwanza na ya mwisho hadi sasa , ameashiria kuwa Bayern Munich inaweza kutoroka na taji la Champions League msimu huu.
Bayern yaweza kunyakua taji: Chalton
Iwapo natakiwa kutaja timu moja , naweza kuitaja Bayern Munich kushinda Champions League, amesema mchezaji huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 75.
Mchezaji huyo wa zamani wa Manchester United , ambaye alikuwamo katika kikosi kilichonyakua ubingwa wa dunia mwaka 1966, amesema mahasimu wa Bayern Munich katika Bundesliga , Borussia Dortmund nayo pia inaweza kufika katika fainali ya Champions League katika uwanja wa Wembley hapo Mei 25.
Schalke 04 walibaki midomo wazi jana wakitafakari kilichowapata hadi kuondolewa tonge mdomoni baada ya kubandikwa mabao 3-2 nyumbani dhidi ya Galatasaray ya Uturuki. Baada ya sare ya bao 1-1 ugenini , Schalke ilikuwa inaonekana kurejea katika robo fainali kwa mara ya tatu kufuatia kufanya hivyo mwaka 2008 na 2011. Lakini Schalke waliporomoka kwa kipigo cha mabao 2-1 hadi mapumziko baada ya mabao mawili katika dakika nane za mwisho wa kipindi cha kwanza "Inauma , Tulicheza vizuri katika michezo yote. "Tumetolewa bila sababu,"
amesema mlinda mlango wa Schalke Timo Hildebrand.
Nayo Barcelona ilito cheche jana baada ya kufuta mabao 2-0 ya AC Milan yaliyopatikana katika mchezo wa kwanza na kupachika mabao 4-0 jana. AC Milan haikuonekana kuwa na jibu lolote katika mchezo huo ambao Lionel Messi alionyesha kuwa yeye ni moto wa kuotea kwa mbali.
Messi binadamu wa ajabu
Gary Lineker mchezaji wa zamani wa Barca na Uingereza ambaye hivi sasa ni mchambuzi wa masuala ya soka , amesema katika ukurasa wake wa Twitter, "Nimefurahi Barca imefanikiwa kusonga mbele. Ulikuwa ni ushindi dhidi ya kila kipingamizi na ushindi kwa mchezo wa mpira.
Marco Materazzi, mlinzi wa zamani wa Inter Milan na Italia, katika Twitter, amesema Habemus Messi ! Wamemuumba kutoka wapi kiumbe huyu wa ajabu? Huyu si binadamu.
Gazeti la Marca la Hispania : Leo, shujaa tena. Messi amejibu wale waliokuwa wakimtilia shaka kwa kuonyesha mchezo wa ajabu.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe
Mhariri: Mohammed Khelef