Tume ya Afrika ndio imekuwa kimbilio la mwisho la haki
26 Aprili 2019Akizungumza katika mkutano wa tume hiyo unaoendelea mjini Sharm El Sheikh nchini Misri, mkurugenzi wa Afrika katika shirika la Human Rights Watch anayeshughulika na masuala ya utetezi, Carine Kaneza-Nantulya alisema uamuzi uliotolewa na baraza kuu la Umoja wa Afrika la kudhibiti majukumu ya tume hiyo unatishia kukikwamisha chombo hicho muhimu sana na kukifanya kama kitu kisichofaa.
Carine alisema Tume ya Afrika ndio imekuwa kimbilio la mwisho kabisa la utetezi wa haki kwa kesi nyingi zisizohesabika zinazowasilishwa na raia kutoka kwa mataifa yanayokiuka haki zao.
Wakiunga mkono taarifa hiyo, viongozi wa mashirika ya kijamii na watetezi wa haki za binadamu kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni walisema uamuzi wa Umoja wa Afrika utainyanga'nya tume hiyo uhuru wa kuweza kuhakikisha viwango vya haki za binadamu vinatimizwa na vilevile kuwachukulia hatua viongozi wa mataifa wanachama wanaokiuka haki hizo.
Mwezi Juni mwaka jana, baraza kuu la Umoja wa Afrika linalohusisha mawaziri wa mambo ya kigeni kutoka kwa nchi wanachama, walitangaza kwamba tume hiyo ina uhuru wa utendaji kazi ila sio uhuru wa kupingana na Umoja wa Afrika iliyoiunda. Pamoja na hilo waliamua kuzirekebisha tena kanuni za namna tume hiyo inavyotoa vibali kwa waangalizi wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kwa utaratibu unaotumiwa na umoja huo kutoa vibali hivyo ambapo unazingatia maadili na tamaduni za Kiafrika.
Mkurugenzi mkuu wa shirika linalounganisha Umoja wa Afrika na makundi ya kijamii barani Afrika, Pan-African Citizen Network, Achieng Akena alisema viongozi wa kisiasa wa mataifa wanachama wanaiona tume hiyo kuwa tishio kwa uongozi wao usiopingwa kwa sababu ina nguvu katika kuwashinikiza kuwajibika katika mikataba ya sheria ya kuwatendea haki waathirika.
Kwa zaidi ya miaka 30, Tume ya Afrika imetanua mipaka yake ya haki za binadamu kote barani Afrika kupitia maamuzi yake muhimu. Imeweza kupokea zaidi ya kesi 400 kufikia mwaka 2015 na kufanya maamuzi katika kesi 235, japokuwa maamuzi ya kesi hizo yanatekelezwa baada ya kupitishwa katika mkutano wa viongozi wakuu wa Umoja wa Afrika na serikali husika.
Karibu kesi hizo zote zimewasilishwa na raia kibinafsi ama makundi yasiyokuwa ya kiserikali.
Tume hiyo pia inalinda haki za wanawake na kuhimiza usawa wa kijinsia barani Afrika ambapo Agosti mwaka 2003 ilizitia hatiani serikali ya Rwanda, Burundi na Uganda kwa kuvipata na makosa vikosi vya majeshi vilivyopelekwa mashariki mwa mikoa ya Jamhuri ya Kidemokasi ya Kongo mwaka 1998 ya ubakaji mkubwa na kuwajeruhi vibaya wanawake na wasichana miongoni mwa ukiukaji mwengine wa haki.
(HRW)