1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Azerbaijan inawaomboleza waathirika wa mkasa wa ndege

26 Desemba 2024

Azerbaijan inafanya maombolezo ya kitaifa kufuatia mkasa wa ndege uliowauwa watu 38 katika Siku Kuu ya Krismasi. Uchunguzi unaendelea kubaini kwa nini ndege ya abiria iliyoruka kutoka Baku ilianguka nchini Kazakhstan.

https://p.dw.com/p/4oaRq
Mabaki ya ndege ya Azerbaijan Airlines
Ndege ya Azerbaijan Airlines ikiwa na watu 67 ilianguka nchini Kazakhstan na kuuwa watu 38Picha: Azamat Sarsenbayev/REUTERS

Bendera nchini Azerbaijan zinapepea nusu mlingoti, huku matukio yote ya kitamaduni yaliyopangwa leo katika kumbi za sinema na za muziki yakifutwa. Chanzo cha kuanguka kwa ndege hiyo ya Shirika la Ndege la Azerbaijan hakijathibitishwa, ijapokuwa maoni kadhaa yametolewa. Abiria 29 walinusurika kifo, baadhi wakiwa na majeraha mabaya.

Soma pia: Ndege ya Azerbaijan yaanguka na kuuwa watu 38

Miili ya abiria waliokufa na wahudumu wa ndege hiyo inasafirishwa hadi Azerbaijan kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa na shirika hilo la ndege na Wizara ya Masuala ya Dharura ya Azerbaijan. Ndege hiyo aina ya Embraer 190 iliondoka Baku jana asubuhi ikiwa na watu 67, wakiwemo wahudumu watano. Ilipangwa kwenda Grozny, mji mkuu wa jamhuri ya Chechnya iliyo chini ya himaya ya Urusi.