BAGHDAD: Makamu waziri wa afya wa Irak atekwa nyara
20 Novemba 2006Duru za usalama nchini Irak, zimesema kuwa watu waliokuwa wamevalia sare za kijeshi wamemteka nyara makamu waziri wa afya wa Irak, Ammar al-Assafar kutoka nyumbani kwake katika mji mkuu wa Irak, Baghdad. Tukio hilo limetokea siku chache baada ya makumi ya wafanyakazi kutekwa nyara kutokoka kwenye taasisi ya utafiti na watu waliokuwa wamevalia sare za kijeshi. Siku ya jana ilishuhudia machafuko makubwa ambapo watu kiasi ya 50 waliuawa katika mashambulio mbali mbali nchini humo. Shambulio baya zaidi ambalo lilikuwa la kujitoa mhanga, limewaua wafanyakazi wa ujenzi 22 wakati mtu aliyekuwa na bomu ameriripua kati kati mwa mkusanyiko wa wafanyakazi hao. Katika mji mkuu Baghdad, kulitokea mashambulizi manne tofauti ambapo kwa uchache watu 20 wameuawa na wengine kiasi ya 50 kujeruhiwa.
Mbali na hayo, maiti za watu 56 waliouawa wengi wao baada ya kuteswa, zimegunduliwa katika miji mitatu nchini humo Irak.