1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Balozi wa India nchini Uingereza achaguliwa katibu mkuu wa Commonwealth

24 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/CSgZ

Jumuiya ya madola Commonwealth imemteua balozi wa India nchini Uingereza, Kamlesh Sharma, kuwa katibu mkuu mpya. Viongozi wa serikali ya jumuiya hiyo wamemchagua Sharma bila kupingwa kuchukua nafasi ya waziri wa zamani wa mashauri ya kigeni wa New Zealand, Don McKinnon, anayeondoka baada ya kushikilia wadhifa huo kwa miaka minane. Wapinzani wakuu wa Sharma walikuwa waziri wa kigeni wa Malta, Micheal Frendo na Mohan Kaul, raia wa Uingereza. Wakati huo huo, polisi nchini Uganda waliwapiga waandamanaji kandoni mwa mkutano wa jumuiya madola, Commonwealth, mjini Kampala. Afisa mmoja wa polisi na raia walijeruhiwa vibaya baada ya polisi kulishambulia kundi la waandamanaji waliopinga ukiukaji wa haki za binadamu. Baadhi ya waandamanaji waliwapiga mawe na kuwarushia chupa polisi. Maafisa wa polisi wamejitetea wakisema waandamanaji hao walikuwa wameondoka eneo rasmi lililotengengwa kwa ajili ya kufanyia maandamano. Wapinzani wa rais wa Uganda, Yoweri Museveni, wanaishutumu jumuiya ya madola kwa kupuuza haki za binadamu nchini Uganda. Viongozi wanaohudhuria mkutano wa Commonwealth mjini Kampala jana walijadili njia za kuendeleza demokrasia, kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria.