1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ban ki Moon akasirishwa na visa vya ubakaji, DRC

25 Agosti 2010

Uchunguzi wa visa vya ubakaji wazinduliwa leo mashariki mwa Jamhuri hiyo.

https://p.dw.com/p/OvWY
Bw Ban ki Moon amemtuma mjumbe wake achunguze hali ilivyo katika taifa hilo.Picha: picture-alliance/ dpa

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban ki Moon ameelezea kukasirishwa kwake na visa vya ubakaji katika eneo la mashariki ya Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo vinavyofanywa na waasi wa Kihutu.

Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Martin Nesirky alisema kiasi ya raia 154 katika Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo walibakwa na kushambuliwa katika uvamizi wa waasi wa Kihutu kutoka Rwanda. Maafisa wengine wa Umoja wa huo wamesema wanawake 179 wamebakwa kwa wiki za hivi karibuni.

Bw Nesirky alisema hiyo ni mfano mwingine wa jinsi viwango vya ubakaji na ukosefu wa usalama vinavyoendelea kulisibu taifa hilo.

Na kutokana na hayo, Bw Nesirky alisema katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon amemtuma Atul Khane, naibu wake anayeshughulikia operesheni za kulinda amani nchini Congo aelekee nchini humo.

Mwakilishi wa katibu mkuu huyo anayeshughulikia masuala ya ukatili wa kimapenzi, Margot Wallstrom amewekwa kusimamia idara ya Umoja huo unaoshughulikia matukio nchini Congo.

Leo misheni ya uchunguzi itazinduliwa mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo ili kuchunguza visa vya ubakaji wa wanawake 200 katika vijiji 15. Timu ya pamoja ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia haki za binaadamu imewatambua washukiwa wa visa hivyo vya ubakaji wakiwemo wapiganaji wa uhuru wa Rwanda na waasi wa kundi la Mai Mai Cheka. Msemaji wa katibu mkuu, Bw Nesirki amesema waathirika wa ubakaji wanaendelea kupata matibabu na ushauri.

Kulingana na Will Cragin wa shirika la kimataifa la madaktari, IMC, kati ya tarehe 30 mwezi Julai mwaka huu na tarehe 3 mwezi Agosti, kiasi ya watu kati ya 200 na 400 waliojihami waliuvamia mji wa Luvungi katika mkoa wa Kivu ya kaskazini amabyo inasifika kwa utajiri wa madini. Eneo hilo linadhibitiwa na waasi ambao kwa kawaida hupora vijijini na kuwasumbua raia.

Wanawake wengi hubakwa na kati ya wanaume wawili au sita mbele ya familia zao majumbani. Kulingana na ripoti ya pamoja ya shirika la Oxfam na mradi wa kiutu wa Harvard uliotolewa mwezi Aprili, asilimia 60 ya visa vya ubakaji katika Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo hutekelezwa na wanajeshi na mara nyingi huwa nyumbani.

Margot Wallstrom, mwakilishi wa katibu wa Umoja wa Mataifa kuhusu dhuluma za kimapenzi, awali aliitaja Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo kama ’mji mkuu wa ubakaji’ duniani.

Zaidi ya wanawake laki mbili wamebakwa katika taifa hilo la Afrika ya kati katika kipindi cha miaka 14 ya vita na afisa huyo wa ngazi ya juu alipohojiwa na shirika la habari la IPS alikiri hiyo ni idadi ya chini.

Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani katika Jamhuri hiyo, kwa kulipa uzito tatizo la ubakaji, sasa wameongeza operesheni zao katika jitihada za kupunguza visa hivyo kwa kupiga doria zaidi na kuwasindikiza wanawake wanapkwenda kwenye zahanati au sokoni.

Mwandishi, Peter Moss /AFP/ IPS

Mhariri, Abdul-Rahman Mohammed