Baraza la Usalama la UM kuiwekea vikwazo Sudan Kusini
1 Desemba 2016Marekani inahangaika kuweza kupata idadi ya kutosha ya kura zinazohitajika kwa ajili ya baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuweka vikwazo dhidi ya Sudan Kusini huku Umoja wa Mataifa ukionya kuhusu uwezekano wa mauaji wa kimbari katika taifa hilo jipya duniani.
Azimio hilo linahitaji kura tisa na bila kupingwa kwa kura ya turufu ili kuweza kupitishwa, lakini wanadiploamsia waandamizi wa Umoja wa Mataifa, wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina, wamesema hadi sasa ni wajumbe saba tu wanaokubali mswada huo, wakati wajumbe wanane waliobaki wanapanga kujitoa kupiga kura ama kupiga kura ya hapana.
Wakati Urusi na China zina wasiwasi juu ya iwapo kuweka vikwazo vya silaha kunaweza kufikia hali ya amani wakati nchi hiyo imetapakaa silaha, wanadiplomasia hawatarajii nchi hizo kuzuwia hatua hiyo iwapo itafikishwa katika baraza hilo kupigiwa kura.
Wanadiplomasia hao wamesema kuna matumaini kwamba Malaysia, Japan, Senegal na Angola zinaweza kushawishiwa kupiga kura kuidhinisha azimio hilo badala ya kujizuwia kupiga kura iwapo mswada huo utapigiwa kura.