Baraza la usalama la UN laitaka serikali na waasi burundi kutekeleza makubaliano
23 Mei 2008NEW-YORK
Baraza la usalama la Umoja wa mataifa limeitaka serikali ya Burundi na makundi ya waasi kutekeleza kikamilifu makubaliano ya amani yaliyotiwa saini miezi 19 iliyopita.Pamoja na kutolewa wito huo na Umoja wa mataifa maafisa nchini Burundi wamefahamisha kwamba jeshi limeanzisha opresheni nyingine dhidi ya ngome za waasi mashariki ya nchi licha ya kuanzishwa mazungumzo juu ya utekelezaji wa usitishaji mapigano na waasi wa kundi la FNL.Afisa mmoja wa serikali Maximmilien Ngendakuriyo amefahamisha kwamba wanajeshi wamewavamia waasi wa FNL hapo jana katika maeneo ya Mbare na Gasarara kilomita tano kutoka mji mkuu Bujumbura.Msemaji wa jeshi Adoplhe Manirakiza amesema hakuna mtu aliyejeruhiwa ingawa opresheni hiyo inaendelea.Opresheni hiyo dhidi ya FNL ndio kubwa zaidi kuwahi kufanywa tangu yalipoanza jumatatu mazungumzo kuhusu utekelezwaji wa mpango wa kusitisha mapigano.