Baraza la Usalama latoa mwito wa kufanyika mazungumzo Jamhuri ya Afrika ya Kati
5 Januari 2013.Baraza la Usalama limeurudia mwito wake wa kufanyika mazungumzo ili kuutatua mgogoro wa Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Wakati huo huo msemaji wa Rais Francois Bozize ameshaeleza mapema kwamba kwenye mazungumzo na waasi, Rais huyo atayakataa matakwa ya waasi hao ya kuondoka madarakani. Msimamo huo wa serikali unaongeza uwezekano wa kuanza tena kwa mapigano katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine limetoa mwito kwa pande zote juuya kutafuta suluhisho kwa njia ya mazungumzo, madhal hali iliyopo haiwezi kutatuliwa kwa njia ya kijeshi.
Waasi wa mfungamano unaoitwa Seleka walisonga mbele hadi karibu na mji mkuu mnamo wiki hii kabla ya kuukubali mwito wa jumuiya ya kimataifa juu ya kufanya mazungumzo. Waasi hao wanamlaumu Rais Bozize kwa kushindwa kuyatekeleza makubaliano ya amani yaliyofikiwa baina yao na serikali katika siku za nyuma.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limezitaka pande zote zinazohusika na mgogoro wa Jamhuri ya Afrika ya Kati zitatafute suluhisho la amani kwa kufanya mazungumzo ya kujenga,bila ya kuweka masharti. Mazungumzo hayo yanapangwa kufanyika kuanzia tarehe 8 katika mji wa Libreville kwa udhamini wa Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika ya Kati,ECCAS.
Hata hivyo waasi wa Seleka wamesema kwamba bado hawajapewa taarifa juu ya mazungumzo hayo. Msemaji wa waasi Eric Massi ameeleza mjini Paris kwamba hawajapata habari zozote juu ya mkutano huo unaopangwa kufanyika chini ya udhamini wa jumuiya ya ECCAS.
Lakini duru za ECCAS zimeliambia Shirika la habari la AFP kuwa ujumbe wa waasi, ikiwa pamoja na msemaji wao Eric Massi utawasili Libreville hapo kesho kabla ya kuanza kwa mkutano hapo tarehe 8 na wajumbe wa serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati. Waasi wa Seleka wana mashaka iwapo Rais Bozize anayo nia ya dhati juu ya pendekezo lake la kugawana mamlaka na waasi.
Waasi hao wanamtaka Rais huyo aondoke madarakani. Lakini ofisi ya Rais imesema matakwa ya waasi hayakubaliki. Mshauri wa Rais ameeleza kwamba matakwa ya waasi juu ya Rais Bozize kuondoka madarakani siyo jambo la kujadiliwa.
Waasi wa mfungamano wa Seleka walianzisha mashambulio tarehe 10 Desemba kutokea kaskazini na walisonga mbele katika sehemu nyingi za nchi kabla ya kuamua kusimamisha hatua zao za kusonga wakati wakiwa wameshafika karibu na mji mkuu Bangui.Kutegemea na yatakayojiri kwenye mazungumzo waasi wamepiga kambi katika mji wa Sibut umbali wa kilometa 160 kaskazini ya mji mkuu Bangui.
Mwandishi:Mtullya Abdu/RTRE/AFP/
Mhariri:Sekione Kitojo