Barca yapangwa tena na PSG hatua ya mtoano
14 Desemba 2020Mtanange kati ya Lionel Messi na Barca na makamu bingwa wa mwaka jana PSG ni marudio ya mechi yao ya mchujo mwaka wa 2017 ambayo Barca walipindua matokeo kwa njia ya kipekee.
Katika droo iliyofanywa leo, mabingwa wa Premier League Liverpool watacheza na RB Leipzig waliofika nusu fainali mwaka jana, mechi itakayomkutanisha kocha Mjerumani Julian Nagelsmann wa Leipzig na Juergen Klopp, kocha nambari moja nchini humo.
Mabingwa mara 13 wa Ulaya Real Madrid watapambana na Atalanta ya Italia, ambao walifika robo fainali mwaka jana. Atletico Madrid watakutana na Chelsea ambapo mshambuliaji Diego Costa atarejea Stamford Bridge. Manchester City ataangushana na Borussia Moenchengladbach, ambao wametinga hatua ya 16 za mwisho kwa mara ya kwanza katika historia ya CL. Juventus yake Christiano Ronaldo itapiga dhidi ya Porto. Mechi hizo za mikondo miwili zitachezwa kuanzia Februari 16
AFP/reuters/DPA/AP