Bayern guu moja katika nusu fainali
3 Aprili 2013Bayern walihitaji tu chini ya dakika moja kuchukua uongozi dhidi ya Juve, kupitia kombora safi la beki chipukizi kutoka Austria David Alaba kabla ya Mjerumani Thomas Müller kufunga la pili katika uwanja wa Allianz Arena muda mfupi baada ya saa moja kukamilika.
Huku timu zote mbili zikiongoza ligi zao za nyumbani, miamba ya Bundesliga Bayern inalenga kufika fainali yao ya tatu ya Champions League katika miaka mine wakati Juventus wakiwa wameshinda mechi zake tano za mwisho za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya timu za Ujerumani. Lakini mabingwa hao wa ligi ya Serie A ya Italia watalazimika kuonyesha mchezo mkali mjini Turin wiki ijayo kama wangetaka kuendeleza rekodi hiyo.
Kiungo Andrea Pirlo amesema wanafahamu kuhusu mchuwano wa marudiano na watafanya kila wawezalo kuyabadilisha matokeo hayo. Pirlo ameomba radhi kutokana na masihara aliyofanya na kusababisha goli la kwanza katika sekunde ya 23 baada ya kupokonywa mpira na Bastian Schweinsteger. Amekiri kuwa Bayern walicheza vyema katika mchuwano mzima na ikawa vigumu kwao kucheza mchezo wao wa kawaida. Ushindi wa Bayern ulikuja na thamani yake wakati kiungo Toni Kroos akitarajiwa kuwa mkekani kwa wiki sita kutokana na jeraha. Mfungaji wa goli la pili Thomas Müller anasema ulikuwa mchezo wa kasi sana na washambuliaji wao walisaidia pia katika kuweka ulinzi thabiti, na inasikitisha kuwa hawakufunga goli la tatu.
Jupp adhihirisha uwezo wa mashambulizi
Mkufunzi wa Bayern Jupp Heynckes alidhihirisha uwezo wa mashambulizi ya Bayern kwa kumwacha nje mshambuliaji raia wa Peru Claudio Pizzaro, licha ya nyota huyo kufunga magoli manne katika ushindi wao wa mabao tisa kwa mawili dhidi ya Hamburg Jumamosi iliyopita, huku Mario Manzukic akianzishwa kama mshambuliaji pekee…..
Nyota wa Brazil Luiz Gustavo alivaa viatu vya Javi Martinez na akashirikiana na Bastian Schweinsteiger wakati Juventus ikiwatumia washambuliaji Alessandro Matri na Fabio Quagliarella. Giorgio Chiellini, Stephen Lichsteiner na Claudio Marchisio walishirikishwa katika kikosi cha kocha Antonio Conte cha mfumo wa 3-5-2.
Jeraha la Kross lilisababisha mabadiliko kwa upande wa Bayern, wakati Arjen Robben akiwekwa ubavu wa kulia naye Müller akisonga katikati ya uwanja naye Franck Ribery akiwekwa ubavu wa kushoto.. Ribbery na Robben walimfanyisha kazi ya ziada Buffon wakati Bayern wakitafita goli la tatu bila kufua dafu.
Mjini Paris, Ufaransa, Barcelona walikabwa na Paris Saint Germain kwa kutoka sare ya magoli mawili kwa mawili. Mkufunzi wa PSG Carlo Ancelotti aliwashangaza wengi kwa kumwanzisha mchezoni David Beckham mwenye umri wa miaka 37 ambaye alikuwa na usiku mgumu. Lionel Messi alifungua ukurasa wa magoli baada ya kudokolewa pasi ya kiufundi kutoka kwa Dani Alves. Kisha nyota huyo Muargentina akatolewa uwanjani katika kipindi cha pili kutokana na jeraha la misuli ya mguu. Zlatan Ibrahimovic aliwasawazishia PSG ijapokuwa alionekana kuwa ameotea… Barca walipewa penalti baada ya mlinda lango wa PSG kumtega Alexis Sanchez..na Xavi akafanya mambo kuwa mawili kwa moja.
Hata hivyo, PSG wakakataa kulala chini na kufa, na katika dakika za majeruhi, Blaise Matuidi akafanya mambo kuwa mawili kwa mawili baada ya kombora lake kumzidi maarifa kipa Victor Valdes ambaye angeokoa kwa urahisi. Katika mechi za leo, Borussia Dortmund watacheza ugenini dhidi ya Malaga nchini Uhispania, wakati Real Madrid wakiangushana na Galatasaray wa Uturuki….
Mwandishi: Bruce Amani/APE
Mhariri: Oummilkheir Hamidou