Bayern kuonyesha ubabe dhidi ya Juventus
1 Aprili 2013Wakati Bayern, mabingwa watarajiwa wa ligi ya bundesliga Ujerumani, wakipambana na Juve, mabingwa watarajiwa wa Italia, wakijipiga kifua kutokana na ushindi wao wa magoli tisa kwa mawili dhidi ya watani wao wa jadi SV Hamburg siku ya Jumamosi, Barcelona na Paris St Germain, timu nyingine zinazotarajiwa kutwaa ubingwa wa Laliga na Ligue 1, zinakutana katika mechi ya kusisimua ya mkondo wa kwanza mjini Paris.
Real Madrid wanawaalika viongozi wa ligi ya Uturuki Galatasaray wakati Malaga wanaoshikilia nafasi ya tatu nchini Uhispania, wakiwaalika Borussia Dortmund ambao wamepokonywa taji na Bayern, lakini wanafanya vyema katika kinyang'anyiro hiki.
Tano kati ya timu nane zilizofuzu katika robo fainali, zinaongoza ligi zao za nyumbani na zinaonekana kutwaa ushindi kabla ya msimu kukamilika, hali inayozipa nafasi ya kuangazia tu macho yao katika Champions League kama zitafuzu katika nusu fainali. Bayern wako pointi 20 mbele ya Borussia nchini Ujerumani na wangetawazwa washindi wa Bundesliga Jumamosi mwishoni wma wiki, baada ya kuwasambaratisha mabingwa wa zamani wa Ulaya Hamburg, hadi pale Robert Lewandowski alipofunga goli lililoipa Dortmund ushindi wa mbili moja dhidi ya VfB Stuttgart.
Juve waliwashidna Inter Milan magoli mawili kwa moja na kusonga pointi 11 kileleni mwa Sierie A mbele ya AC Milan, wakati Barca wakipanua uongozi wa Laliga na pointi 13 mbele ya Real Madrid.
Galatasaray na PSG zinashikilia uongozi nchini Uturuki na Ufaransa, na, wakati Real na Dortmund zikionekana kuishiwa matumaini ya kuhifadhi mataji yao, zinajihakikishia kumaliza katika nafasi nzuri ili kurejea tena katika Ligi ya Mabingwa msimu ujao.
Licha ya kutokuwepo na timu yoyote ya Premier League ya England katika timu nane za mwisho kwa mara ya kwanza tangu 1996, fainali ya mwaka huu uwanjani Wembley jijini London huenda ikawa “Classico” baina ya Real na Barca au fainali ya timu zote za Ujerumani kati ya Borussia na Bayern.
Mchuwano kati ya Real Madrid na Galatasaray unawaleta pamoja watu watatu wanaofahamiana, Jose Mourinho, Didier Drogba na Wesley Sneijder. Mourinho anatarajiwa kuongoza Real kunyakua taji lake la kumi barani Ulaya na kuwa mkufunzi wa kwanza kunyanyua taji hilo na vilabu vitatu tofauti, baada ya kufanya hivyo na Inter na Porto.
Alifanya kazi na Drogba akiwa katika klabu ya Chelsea na Sneijder alikuwa katika timu ya Inter iliyoshinda Champions League mwaka wa 2010, lakini sasa Sneijder na Drogba wako Galatasaray. Mechi za mikondo ya pili zitachezwa wiki ijayo huku nusu fainali zikichezwa mwishoni mwa mwezi Aprili na mwanzoni mwa Mei. Fainali itakuwa uwanjani Wembley mnamo Mei 25.
Mwandishi: Bruce Amani/DPA/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef