1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern kupambana na Juventus Champions League

Admin.WagnerD14 Desemba 2015

Timu 16 zilizosalia katika awamu ya mtoano ya UEFA Champions League , Bayern kupambana na Juve na mabingwa Barcelona ina miadi na Arsenal London.

https://p.dw.com/p/1HNAd
Champions League Auslosung
Upangaji wa timu zitakavyopambana katika awamu ya mtoano ya Champions LeaguePicha: Getty Images/AFP/F. Coffrini

Mabingwa wa Ulaya Barcelona watalazimika kuwabwaga viongozi wa ligi ya Uingereza Premier League Arsenal katika awamu ya mtoano ya Champions League ili kujihakikishia tikiti ya kucheza katika robo fainali ya msimu huu ya Champions League , baada ya kura ya kuzipambanisha timu zilizosalia katika kundi la timu 16 bora barani Ulaya leo mjini Nyon nchini Uswisi.

Vigogo wa Ufaransa Paris Saint-Germain wamepangiwa kupimana ubavu na mabingwa wa mwaka 2012 Chelsea ya Uingereza kwa msimu wa tatu mfululizo, wakati Bayern Munich itakumbana na Juventus Turin iliyofikia fainali msimu uliopita.

Mabingwa mara kumi wa ligi hiyo ya Ulaya Real Madrid ina miadi na Roma ya Italia wakati Manchester City itakumbana na Dynamo Kiev ya Ukraine katika kinyang'anyiro cha kuwania kuingia duru ya robo fainali. Gent ya Ubelgiji itaikaribisha Wolfsburg ya Ujerumani , wakati PSV Eindhoven ina miadi na Atletico Madrid ya Uhispania. Benfica Lissabon ya Ureno itaoneshana kazi na Zenit St. Petresburg.

Champions League Auslosung
Timu zilivyopangwa kwa ajili ya Champions LeaguePicha: Getty Images/AFP/F. Coffrini

Kura hiyo ya kuzipanga timu hizo ilifanyika katika makao makuu ya shirikisho la kandanda barani Ulaya UEFA mjini Nyon, nchini Uswisi. Michezo hiyo itafanyika kati ya Februari 16 na Machi 16

Klopp kurejea Ujerumani

Na katika Europa League kocha wa zamani wa Borussia Dortmund Jürgen Klopp atarejea nyumbani wakati timu yake ya sasa Liverpool itakapopambana na Augsburg na Borussia Dortmund imepangiwa kuoneshana kazi na Porto ya Ureno.

Manchester United iliyoporomoka kutoka Champions League imepangiwa kukumbana na Midtjyaland ya Denmark na Tottenham Hotspurs itaumana na Fiorentina ya Italia.

Schalke 04 itakwaana na Shakhtar Donetsk na Bayer leverkusen itapambana na Sporting Lisbon.

Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre /dpae / afpe
Mhariri:Yusuf Saumu