1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern mabingwa wa mzunguko wa kwanza wa Bundesliga

23 Desemba 2024

Ligi kuu ya kandanda Ujerumani - Bundesliga imeingia mapumziko mafupi ya msimu wa baridi kali. Vilabu vimeenda kujipanga upya kabla ya kurudi tena viwanjani Januari 10 mwakani kuanza mzunguko wa pili wa msimu.

https://p.dw.com/p/4oWsS
Bayern Munich
Bayern Munich wanaongoza msimamo wa Bundesliga na pengo la pointi nne dhidi ya nambari mbili LeverkusenPicha: Hasan Bratic/IMAGO

Bayern Munich ndio mabingwa wa mzunguko wa kwanza - Herbstmeister kama inavyojulikana hapa Ujerumani. Ni baada ya kuinyeshea RB Leipzig 5 – 1. Hata hivyo kocha Vincent Kompany alipata ugumu kutafakari juu ya ushindi wa timu yake kufuatia shambulizi kwenye soko la Krismasi nchini Ujerumani na kusababisha vifo vya watu watano na wengine kadhaa kujeruhiwa. "Nadhani timu na vijana walifanya kazi kubwa. Lakini mwishowe, ni usiku mgumu kwetu kuzungumzia kandanda bila shaka. Nilipata habari kuhusu kilichofanyika sio mbali sana kutoka hapa. Na mwisho wa yote, kwa sasa ni hisia za huzuni na kuhakikisha kuwa, kwa kumaliza mwaka wa 2024, tunaweza kuanza mwaka mpya wa 2025 kukiwa na amani kwa ujumla."

Leverkusen waliwachabanga Freiburg
Florian Wirtz alikuwa na mchezo mzuri sana wakati Leverkusen ikiibamiza Freiburg 5 - 1Picha: Sascha Weiz/pepphoto/IMAGO

Soma pia:Kane atupia hat trick dhidi ya Augsburg wakati Bayern ikitanua mwanya kileleni

Bayern sasa wana pointi 36, nne mbele ya mabingwa watetezi Bayer Leverkusen, ambao baada ya kujikwaa kwenye mechi kadhaa, wamerejea katika mbio za ubingwa. Waliwafumua Freiburg 5 – 1 katika mechi ambayo Florian Wirtz alionesha umahiri wake, hata ingawa Patrick Schick alipachika mabao manne katika mechi hiyo. Kocha Xabi Alonso aliipongeza timu yake akisisitiza kuwa mtanange huo ulikuwa mgumu zaidi kuliko matokeo yanavyoonesha "Tunataka kuwa bora. Tunataka kuendelea kucheza vizuri, kuonyesha tunajiamini, kuwa na ushindani. Na kwa hilo, tutakuwa na nafasi zaidi za kushinda mechi. Acha tuone kuona tulipo sasa. Lakini hatufikirii huko mbele. Hatufikirii kuhusu mwezi Mei. Tutafikiria juu ya kile kitakachokuja Januari kwa sababu itakuwa kazi ngumu tena. "

Borussia Dortmund iliumaliza mwaka wa 2024 kwa ushindi wa 3 – 1 dhidi ya VfL Wolfsburg, lakini kocha Nuri Sahin ameihimiza timu yake kuwa thabiti zaidi ili kurejea katika nafasi nne za juu za Bundesliga katika nusu ya pili ya msimu.

Ushindi huo wa kwanza wa Dortmund wa ugenini msimu huu kwenye Bundesliga ulimaliza mfululizo wa mechi tatu bila kushinda, na kuwapandisha hadi nafasi ya sita, ambayo ni ya mwisho kufuzu kwa soka la Ulaya. Kocha Sahin alilalamika kuwa timu yake haipo kwenye nafasi za juu za jedwali.