Bayern Munich haijakaa sawa baada ya Ancelotti
2 Oktoba 2017Willy Sagnol hakutaka kufanya makosa. Lakini kocha huyo wa mpito wa mabingwa watetezi wa Bundesliga Bayern Munich katika mchezo dhidi ya Hertha BSC Berlin alishindwa kuhimili vishindo vya wenyeji na kupoteza uongozi wa mabao 2-0 na hatimaye kuridhika na suluhu ya mabao 2-2 , ikiwa ni mara ya pili kwa Bayern kufanya hivyo katika muda wa wiki mbili.
Mshambuliaji wa Bayern Munich Thomas Mueller alikuwa na haya ya kusema.
"Tumefadhaishwa sana na kuvunjika moyo, kwamba kwa mara ya pili hatukuweza , kulinda uongozi wetu wa mabao 2 na kuwa ushindi mwishoni."
Kocha wa mpito Willy Sagnol amelalamika kwamba , walihitaji katika mchezo huo wachezaji ambao wako katika hali nzuri kimchezo baada ya mchezo dhidi ya Paris Saint Germain katikati ya wiki iliyopita kwa kuwa mchezo huo ulikuwa mgumu na baadhi ya wachezaji walikuwa wamechoka.
Na pia mvutano wa kuwania madaraka chini ya uongozi wa Ancelotti ulileta athari kubwa katika timu.
Mchezaji wa ulinzi wa Hertha Berlin Niklas Stark anasema.
"Tumepata pointi moja. Kwasababu unapokuwa nyuma kwa mabao 2-0 dhidi ya Bayern, ni rahisi kukubali kushindwa."
Borussia Dortmund imeshikilia uongozi wa ligi ya Bundesliga ikiwa na pointi 19 na mabao 21, wakati Bayern Munich kwa kutoka sare na Hertha Berlin imechupa hadi nafasi ya pili ikiwa na pointi 14 pointi 5 nyuma ya Dortmund.
TSG Hoffenheim imeteremka hadi nafasi ya tatu kutokana na kipigo cha mabao 3-2 jana Jumapili dhidi ya FC Freiburg. Florian Niederlechner mshambuliaji wa Freiburg anazungumzia mchezo huo.
"Ni hali ya kusisimua sana. Tumeonesha mchezo mzuri katika michezo yetu miwili iliyopita, lakini kwa bahati mbaya hatukuweza kufaidika. Kwa bahati nzuri leo tumefanikiwa. Ni muhimu sana. Pointi zetu tatu za kwanza , kila mtu anatambua sasa kuwa kikosi chetu kiko hai."
FC Kolon haijaanza vizuri msimu huu na hadi sasa hakujapatikana jibu mjarabu kuhusu masaibu yanayokikumba kikosi cha kocha Peter Stoeger.
Lakini mwenyewe bado ana matumaini.
"Kwangu mimi inatia moyo, kuona vijana wangu wana mwelekeo sahihi, kuhusiana na kila mara tunachowaambia. Nikiangalia kwa undani , wamefadhaika , na vipi wanavyolalamika, naona hali ni ngumu, kuweza kubadilisha hali hiyo moja kwa moja."
FC Kolon ina pointi moja tu na inasubiri kwa hamu ushindi wake wa kwanza katika msimu huu wa ligi ya Bundesliga na inashika mkia baada ya michezo 7.
Wakati huo huo Bayern Munich inatarajia kukosa huduma ya mshambuliaji wa pembeni wa siku nyingi Frank Ribery kwa zaidi ya miezi mitatu kutokana na kukatika kwa misipa katika goti lake la mguu wa kushoto.Ribery mwenye umri wa miaka 34 alisaidiwa wakati akitoka nje ya uwanja katika mchezo ambao Bayern ilitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Hertha Berlin.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / rtre / afpe / ape
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman