Bayern Munich mabingwa Champions League
26 Mei 2013Ni Arjen Robben ndiye aliyepachika bao la ushindi katika dakika ya 89 na kuipatia Bayern Munich ushindi muhimu dhidi ya mahasimu wao Borussia Dortmund jana Jumamosi (25.05.2013), baada ya mchezo wa kuvutia wa fainali ya ChampionsLeague katika uwanja wa Wembley mjini London.
Wakati muda wa nyongeza ukipiga hodi, Robben alipokea pasi ya kisigino kutoka kwa Frank Ribery, akamkwepa Mats Hummels na kuuweka mpira wavuni akimwacha Roman Weidenfeller bila majibu na kuipatia Bayern Munich taji lake la tano la mabingwa wa Ulaya.
Ulikuwa muda uliokuwa unasubiriwa mno kwa Bayern na Robben baada ya kushindwa kulitwaa taji hilo katika fainali za mwaka 2010 na 2012, wakati walipobwagwa kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Chelsea London katika uwanja wake wa nyumbani.
"Kipindi changu chote cha kucheza soka kilipita katika mawazo yangu wakati nilipopachika bao hilo. Ni hali ya kipekee kabisa unayoweza kuihisi, huwezi kuielezea," Robben amesema.
Heynckes amwagiwa sifa
Lakini zaidi ni kocha wa Bayern Munich, Jupp Heynckes, ambaye alimiminiwa sifa tele baada ya timu yake kunyakua taji hilo. Rais wa klabu hiyo, Uli Hoeness, alimwagia sifa Heynckes mwenye umri wa miaka 68 ambaye anaweza kushinda mataji matatu na Bayern mwishoni mwa juma lijalo iwapo timu hiyo itaishinda VFB Stuttgart katika fainali ya Kombe la Shirikisho, DFB Pokal.
"Nimefurahi kwamba klabu hii sasa iko juu kabisa katika Ulaya," Hoeness amesema.
"Jupp amefanya kazi nzuri sana. Kuiweka timu hii na nyota wake wote katika hali sahihi na kuifanya kuendelea kufanya vizuri katika kiwango cha juu kabisa ni mkono wa Jupp Heynckes."
Mchezaji wa kiungo wa Bayern Munich, Bastian Schweinsteiger, amesema: "Tumekuwa na msimu mzuri sana na Heynckes ana sehemu kubwa katika mafanikio hayo. Anakwenda na wakati na anaongoza akiwa mbele."
Kocha wa Dortmund, Juergen Klopp, alimkumbatia Heynckes baada ya mchezo na alimmwagia sifa tele. "Ni mtu mzuri na muhimu," amesema Klopp na kuongeza kwamba ulikuwa mchezo wenye mambo mengi na mgumu. "Ni matokeo yanayostahili na mliona kuwa pia tulistahili kuwapo katika fainali. Tulikuwa karibu sana na kulibeba taji hili. Nimewaambia wachezaji wangu kuwa tutarejea tena, huenda sio Wembley lakini tutajaribu kurejea tena katika fainali nyingine. Hicho ndicho nilichowaeleza wachezaji."
Naye kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani, Joachim Loew, amesema anaipongeza Bayern kwa ushindi lakini "zaidi ya yote nampongeza Jupp Heynckes." Loew ameuita mchezo huo kuwa fainali ya hali ya juu kabisa ambayo ilikuwa na kila kitu kinachohitajika kutoka katika soka.
"Timu zote zimeonyesha mchezo wa kiwango cha juu na kwamba zilistahili kuwapo katika fainali hii. Timu ambayo ilikuwa katika fainali tatu katika muda wa miaka minne inastahili kushinda ubingwa huu. Huenda ilikuwa kwamba ni zamu ya Bayern mwaka huu," amesema Loew.
Wachezaji maarufu waimwagia sifa Bayern
Ottmar Hitzfeld, ambaye aliwahi kushinda taji hilo akiwa na Borussia Dortmund na Bayern Munich na ambaye hivi sasa ni kocha wa timu ya taifa ya Uswisi, amesema Dortmund walionesha ujasiri wa hali ya juu kabisa.
"Wakati wote walipokuwa na uwezo na nguvu za kuwasukuma mbele walicheza mchezo safi wa kulazimisha na kutoa mbinyo, " amesema Hotzfeld na kuongeza kuwa kila muda ulivyokwenda katika mchezo huo timu iliyokuwa ikipigiwa upatu kutoroka na taji hilo, Bayern, ilikuwa inazidi kuwa na nguvu zaidi. "Uliweza kuhisi nguvu walizokuwa nazo."
Ushindi wa Bayern unamfanya kocha Jupp Heynckes kuwa kocha wa nne kushinda taji hilo akiwa na timu mbili tofauti, baada ya ushindi wa mwaka 1998 akiwa na Real Madrid, wakati akijitayarisha kung'atuka na kumpisha kocha wa zamani wa Barcelona, Pep Guardiola, kuchukua nafasi yake.
Mwandishi: Sekione Kitojo/afpe/dpae
Mhariri: Mohammed Khelef