Bayern Munich pointi sawa na B.Leverksen
8 Februari 2010Bayer Leverkusen, licha ya kutoka sare bao 1:1 na Bochum,ingali inaongoza Bundesliga alao kwa magoli, ikiwa pointi sawa na Bayern Munich.Mabao 2 ya muivory Coast,Didier Drogba, yafungua mwanya wa pointi 2 kileleni kati ya Chelsea na Manchester United.
Kura imepigwa kwa Kombe la Ulaya la Mataifa 2012:je, kocha wa Ujerumani Joachim Loew, atabaki kitini hadi wakati huo ? Nigeria, yamtimua kocha wake Shuaibu Amodu baada ya Super Eagles kumaliza nafasi ya 3 katika Kombe la Afrika la Mataifa nchini Angola.
Tukianza na Bundesliga, mabingwa mara kadhaa wa Ujerumani, Bayern Munich,walisawazisha na kuwa pointi sawa na viongozi wa muda mrefu wa Bundesliga-Bayer Leverkusen.Munich hapo Jumamosi, ililipiza kisasi kwa mabingwa Wolfsburg kwa kuwatandika mabao 3-0.Ilikua mholanzi Arjen Robben alielifumania kwanza lango la Wolfsburg ,hilo likiwa bao lake la 3 katika mapambano 3 mfululizo.Na tangu kujiunga na Bayern Munich kutoka Real Madrid hapo August, mwaka jana, ameshatia mabao 7 katika mapambano 13.Msimu uliopita pale Wiolfsburg ilipokuwa njiani kutwaa ubingwa, iliifedhehsha Munich kwa mabao 5-1.
Mahasimu wao killeni bayer Leverkusen, walitoka sare na Bochum na kupoteza pointi 2.Leverkusen iliondoka sare bao 1:1.Kocha wa Bayer Leverkusen Jupp Hynckes ,aonesha hatahivyo, ameridhika na pointi hiyo moja .Amesema:
"Iwapo tumeshindwa au la, muhimu zaidi hiyo pointi 1 yaweza ikawa muhimu sana katika hesabu ya mwishoni mwa Ligi.Kwani, maarifa yangu kama mchezaji na kocha ,yameonesha wakati mwengine, unavunjika moyo na pointi 1,halafu unaona ndio iliokuokoa."
Stuttgart imeilaza Nuremberg mabao 2-1.FC Cologne ilimudu dakika ya mwisho kusawazisha mabao 3-3 na Hamburg iliomteremsha dakika ya mwisho jogoo lao jipya van Niestelrooy.Hamburg, ikiongoza mabao 3:1,lakini Cologne, haikukata tamaa na katika dakika ya 88 ya mchezo,mmorocco Adil Cihi alisawazisha baada ya mshambulizi Novakovic kuipatia Cologne bao la pili.Hoffenheim wameichapa Hannover 2-1.Werder Bremen ilifungua duru hii ya mwishoni mwa wiki ilipotamba kwa mabao 2:1 mbele ya Hertha Berlin hapo ijumaa.
Katika Premier League-Ligi ya Uingereza,Didier Drogba,wa ivory Coast,iliikandika Arsenal mabao 2:0 jana na kurejea kileleni mwa Premier League.Chelsea ina pointi 58-pointi 2 zaidi kuliko Manchester united,mahasimu wao.Manchrster City wanamkaribisha stadi wa Ufaransa, Patrick Vieira uwanjani kwa mara ya kwanza kesho kwa changamoto dhidi ya Bolton Wanderes.Pigo la mabao 2-1 ililopata Manchester City kutoka Hull City limewakatia tamaa Manchester City kujiunga na timu za kileleni.
Kura ilipigwa jana mjini Warsaw kuamua jinsi timu za ulaya zitakavyoania tiketi zao kufuzu kwa Kombe la Ulaya la Mataifa 2012 litakaloaniwa kwa ubia nchini Poland na Ukraine.Mabingwa Spain wameangukia kundi moja na Jamhuri ya Czech na Scotland.
Makamo-bingwa wa Ulaya,Ujerumani, wako kundi moja na Uturuki na jirani zao Austria na Ubelgiji.
Kocha wa Ujerumani Joachim Loew, ambae wakati huu anazozana na Shirikisho la dimba la Ujerumani (DFB) juu ya mkataba wake mpya alisema hivi juu ya kura ya jana:
"Nadhani Ujerumani na Uturuki ndizo zitakazofuzu kutoka kundi hili."
Nae kocha wa Ubelgiji akasema,
"Ujerumani ni timu kali,lakini timu kama Ubelgiji inavutia sana kucheza kundi moja na Ujerumani."
Huko Afrika ya magharibi, Nigeria,imemtimua kocha wake Shuaibu Amodu na kutangaza orodha fupi ya makocha ambao mmojawao aweza kuwaongoza Super Eagles katika Kombe lijalo la Dunia ,nchini Afrika Kusini, Juni hii ijayo. Amodu amekuwa mashakani hata kabla Nigeria, kumaliza nafasi ya 3 katika Kombe la Afrika la Mataifa mwezi uliopita nchini Angola.
Orodha hiyo ya makocha inaongozwa na Kocha wa sasa wa Urusi,Guus Hiddink,kocha wa Bayern Munich,van Gaal na mfaransa, Bruno Metsu na hata muingereza Peter Taylor.
Amodu ,Novemba mwaka uliopita, aliiongoza Nigeria kufuzu kwa Kombe lijalo la dunia nchini Afrika Kusini.Hatahivyo, wengi hawakufurahishwa na mchezo wa Nigeria chini ya uongozi wake.
Taarifa nyengine kutoka Afrika ya magharibi zasema kwamba, maalfu ya mashabiki wa Togo, waliandamana Jumamosi mjini Lome, wakilalamika kwa timu yao ya taifa kupigwa marufuku kucheza Kombe la Afrika kuanzia 2012 hadi 2014. Waandamanaji walibeba mabiramu yakidai rais wa CAF-Shirikisho la kabumbu la Afrika ,Issa Hayatou kutoka Kameroun,ajiuzulu.
Mwandishi:Ramadhan Ali/DPAE/RTRE
Mhariri:Abdul-Rahman