1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern Munich yapigiwa upatu kuwika tena msimu huu

Oumilkher Hamidou27 Agosti 2010

Mashabiki wa timu iliyonyakua ubingwa mara 22 nchini Ujerumani wataraji timu yao Bayern Munich itanyakua vikombe vyote vitatu msimu huu

https://p.dw.com/p/OxYL
Aliyekua mwenyekiti wa timu ya Bayern Münich,Franz Beckenbauer,mbele ya nembo ya timu hiyo ya kusini mwa Ujerumani,kabla ya wadhifa huo kukabidhiwa Uli HoeneßPicha: AP

Mtu akiwauliza mashabiki na wadadisi kuhusu maoni yao nani ataibuka na taji la ubingwa msimu huu-jibu daima limekua moja tuu-Bayern Munich.Na safari hii pia hali si nyengine.Na hayo si ajabu tukitilia maanani jinsi timu hiyo ya kusini mwa Ujerumani ilivyowika msimu uliopita.

Haiingii akilini kutanguliza pigo mtu akitaka kuizungumzia timu iliyotia fora katika kutwaa mataji ya ubingwa ya ligi kuu ya Ujerumani .Watoto wa FC Bayern Munich walikua msimu uliopita nusra waweke rikodi mpya ya ajabu:Walitwaa taji la ubingwa wa ligi kuu baada ya michuano kabambe kabisa.Wametwaa kombe baada ya kuwatwanga Werder Bremen manne kwa yai.Wamelikosa taji moja tuu kuweza kuvikwa mataji matatu kwa pamoja katika historia yao!Mwishoe lakini katika pambano la fainali la kuania kombe la vilabu bingwa barani Ulaya- Champions League-timu hiyo inayoongozwa na Kocha Louis van Gaal ililazimika kusalim amri mbele ya Inter Mailand.

"Nnahisi tulistahili kushindwa.Tungebidi kuwa katika hali bora zaidi kuweza kuwashinda Inter-na hatukua hivyo."

ameungama hatimae kocha huyo wa kutoka Uholanzi.FC Bayern hawajawahi kuwa wakali kama walivyokua msimu wa kiangazi mwaka huu wa 2010.Licha ya mataji 22 waliyonyakua katika ligi kuu ya Ujerumani,licha ya vikombe 15 vya Ujerumani walivyoshinda,na licha ya kushinda mara nne katika michuano ya Ulaya au Champions League.

Lakini hata kama msimu huu hawajafanikiwa kutwaa taji la Ulaya,watoto wa Munich wamewavutia mashabiki zaidi msimu huu.Mmojawapo ambae daima amekua akipaza sauti ni Uli Hoeneß,aliyewahi wakati mmoja kuichezea timu hiyo na baadae kuwa meneja wake kwa muda wa miaka 30 na kuchaguliwa tangu msimu wa mapukutiko uliopita kuwa mwenyekiti wa timu hiyo ya Bayern Münich.Alipovua jozi ya dimba na kujiunga na uongozi wa timu hiyo,Bayern Munich ilikua takriban muflis.Hii leo anaongoza mojawapo ya vilabu tajiri kabisa vya soka ulimwenguni.

"Daima nimejitahidi kuitumikia Bayern Munich.Daima nimekua nikijaribu kuinyanyua timu hii.Nnaamini,nikitafakari yote niliyoyafanya katika kilabu hii ya Bayern Munich,basi nnaweza kusema sijafanya kazi mbaya."

Alisema Hoeneß alipochaguliwa kuwa mwenyekiti wa timu hiyo.Na nani wakumsuta?Hivi sasa Christian Nerlinger ndie aliyekabidhiwa wadhifa wa Hoeneß kama meneja wa Bayern Munich na kwa kumuajiri Arien Robben,amefanikiwa pakubwa katika uwanja huo.Pamoja na Frank Ribery,Bastian Schweinsteiger,Mark van Bommel na Philipp Lahm wao ndio wanaounda nguzo ya Bayern Munich mpya.

Bayern München : Olli Hoeneß unterstutzt Van Gall, als dieser in der Kritik geriet. Flash-Galerie
Mwenyekiti wa Bayern Munich Uli Hoeneß (kushoto) na kocha wa Bayern Munich Louis van GaalPicha: AP/DW

Kati ya mashabiki wakubwa wa Bayern Munich ni Günther Netzer,ambae japo kama hajawahi kuichezea timu ya FC Bayern Munich lakini ameshawahi kuwa bingwa wa dunia na pengine mchezaji nyota kuliko wote ambao Ujerumani imewahi kuwa nao.

"Kila wakati wamekua wakijitokeza kwa ustadi mkubwa,werevu mkubwa,naiwe mwenyekiti,uongozi au pia aupande wa wachezaji.Ni werevu na ustadi wa hali ya juu.Wameigeuza FC Bayern Munich kuwa timu ya aina pekee nchini Ujerumani na mashuihuri ulimwenguni."

Anasema Günther Netzer.

Kilichowabakia lakini ni kunyakua vikombe vitatu kwa pamoja.Pengine msimu huu watafanikiwa.

Mwandishi :Oelmaier Thobias/ZR/Hamidou,Oummilkheir

Mpitiaji:Mohammed Abdul-Rahman