Bayern Munich yatamba mbele ya Dortmund
9 Februari 2009Mabao ya dakika za mwisho ya Miroslav klose katika lango la Borussia Dortmund yairudisha Bayern Munich kileleni mwa Bundesliga-
Katika Premier League-Manchester united yachukuia usukani na huko Spain, FC Barcelona,yanyakua ushindi wake wa 10 mfululizo kileleni mwa La Liga.
Taifa Stars-timu ya Taifa ya Tanzania yajiandaa kwa kombe la Afrika huko Ivory Coast.
Mabingwa wa Ujerumani -Bayern Munich waliiambia Borussia Dortmund jana usiku kwamba, kutangulia si kufika:Mwishoe,shukurani kwa mabao 2 ya dakika za mwisho ya Miroslav klose, Munich ilitamba kwa mabao 3-1 na sasa iko pointi 1 tu nyuma ya chipukizi waliopanda kutoka daraja ya pili Hoffenheim.
Dortmund iliwapiga mabingwa msumari wa nyuko dakikja 2 tu baada ya dimba kuanza pale Nelson Valdez alipolifumania lango la mabingwa tena nyumbani mwao Munich.
Bao hilo likawa kama kuchokoza nyuki,hujuma kali zilizolengwa katika lanbgo la Dortmund,hazikukawia kuzaa matunda. Mbrazil Ze Roberto alisawazisha kabla Miroslav klose kutia bao la pili na la 3 la ushindi dakika za mwisho na kuvunja ubishi wa Dortmund.
Baada ya kutia mabao hayo, mshambulizi wa timu ya taifa Miroslav klose alisema:
"Ninamshukuru mungu kuwa nilitia mabao,kwani tungehindwa leo au kutoka sare,basi wote wangeuelekeza mkuki kifuani mwangu."
Alisema Miroslav Klose ambae kitambo hakunasa wavu.Akaongeza:
"Najitahidi sana kwa timu yetu na mwishoe hii ni jaza yake."
Ama katika changamoto nyengine ,viongozi wa ligi Hoffenheim walimdu sare ya bao 1:1 kati yao na Borussia Moenchengladbach na sasa wana pointi 39 kwa 38 za mabingwa Bayern Munich.Nafasi ya tatu inanyatia Hertha Berlin huku Hamburg ikiwa nafasi ya 4.
Energie Cottbus ikicheza nyumbani,iliiitikisa Hannover barabara na mwishoe ikaondoka uwanjani na mabao 3-1.Shukurani nyingi ziende kwa mshambulizi wao Dimitar Rangelov kabla ya mwenzake Stansilav Angelov kuizika Hannover katika kaburi waliowachimbia kwa bao la 3.
FC Cologne ilimudu suluhuya mabao 2:2 na Frankfurt.
Mabingwa wa Uingereza, Manchester United, wameparamia kileleni j mwa Premier League jana baada ya Ryan Giggs kulifumania lango la West Ham kwa bao pekee.
West Ham imekuwa ikitia fora sana ikiongozwa na kocha Gianfranco Zola na katika kipindi cha kwanza nusra Manu ikione kilichomtoa kanga manyoya.Lakini, ilichukua hadi dakika ya 62 ya mchezo,kwa Giggs kuvunja ubishi wao kwa bao hilo pekee.
Arsenal imeangukia nafasi ya 5-ikiwa pointi 5 nyuma ya Chelsea.
Chelsea ilimudu suluhu tu 0:0 na Hull City wakati Liverpool waliikomea portsmouth mabao 3-2.Arsenal ilimudu sare 0:0 na Tottenham Hotspurs.Mancherster City iliikomea Middlesbrough.
Katika La Liga-au ligi ya Spain, FC Barcelona inaendelea kunguruma: Kwani, jana iliikomea Sporting Gijon mabao 3-1 huku simba wa nyika-Mkamerun,Samuel Eto-o, akinguruma kwa mabao yake 2.Eto-o sasa anaongoza orodha ya watiaji mabao mengi katika Ligi ya Spain.Barcelona imefungua mwanya wa pointi 12 kati yake na Real Madrid iliotamba nyumbani kwa bao 1:0 mbele ya Racing Santander.
Real hata hivyo, inaonesha sasa iko imara ikinyatia kutoka nafasi ya pili.
Valencia ilichapwa mabao 2 -1 na Real Betis wakati Valencia imeteleza mbele ya Osasuna.
Bao la dakika za mwisho alilotia Christian Poulsen liliipatia Juventus ushindi
wa mabao 2-1 mbele ya Catania.Sasa Juve iko pointi 7 nyuma ya viongozi wa Ligi Inter Milan.Inter iliizaba Lecce mabao 3 bila majibu na sasa yaongoza Serie A-Ligi ya Itali ikiwa na jumla ya pointi 53.AC Milan mahasimu wao wakubwa wa mtaani waliteleza hadi pointi 8 kwa kumudu sare ya bao 1:1 na Reggina inayoburura mkia wa Ligi.
Msimu mpya wa Ligi ya Kenya ulianza rasmi Jumamosi na jumla ya mabao 8 yalitiwa kimiyani.Klabu mpya na chipukizi iliozaliwa kanisani, (Sofapaka )imeanza kutamba.
Tanzania:Taifa Stars inajiwinda kwa safari ya Ivory Coast kushiriki katika kombe la Afrika la wachezaji wasiolipwa.
Kabla ya kuelekea Ivory Coast,Taifa Stars ilifika kisiwani Zanzibar kwa mazowezi na kufuta malalamiko kuwa ni timu ya upande mmoja tu-Tanzania-bara.Tanzania itaondoka Februari 19 kwa safari ya Ivory Coast.