Bayern ni mabingwa wa UEFA Super Cup
31 Agosti 2013Bayern Munich, ikiongozwa na kocha wao mpya, Pep Guardiola, imelipiza kisasi kwa kushindwa na Chelsea katika fainali ya Champions League mwaka 2012 baada ya kuifunga klabu hiyo mabao 5-4 kupitia mikwaju ya penalti kufuatia mtanange wa kuwania kombe la UEFA Super Cup kuishia sare ya mabao 2-2 baada ya muda wa ziada kumalizika.
Bao la Bayern sekunde chache kabla mchezo kumalizika, liliufungua mlango wa kuelekea ushindi kupitia penalti dhidi ya Chelsea chini ya kocha wao mpya, Jose Mourinho. Penalti zote tisa ziliutikisa wavu kabla mkwaju wa penalti wa mchezaji wa Chelsea, Romeu Lukaku, kuokolewa na kipa wa Bayern Munich, Manuel Neuer, na hivyo kuwapa ushindi mabingwa wa Ulaya, Bayern Munich, dhidi ya mabingwa wa ligi ya Ulaya, Chelsea.
Ushindi wa kwanza katika historia
Hii ni mara ya kwanza kwa Bayern Munich kushinda kombe la UEFA Super Cup katika historia yake, baada ya kupoteza fainali nyengine tatu. Fernando Torres aliifungia Chelsea bao la kwanza dakika ya nane ya mchezo, pale alipopewa mpira na Mjerumani Andre Shuerrle. Frank Ribery alisawazisha dakika ya 47 katika kipindi cha pili kupitia mkwaju mkali akiwa mita 25 kutoka lango la Chelsea, mkwaju ambao kipa wa Chelsea, Petr Cech, hakuweza kuuzuia.
"Nina furaha sana kwa ajili ya timu yangu na kocha wangu. Ilikuwa siku maalumu sana kwake katika uhasama wake wa kihistoria na hasimu wake Mourihno," amesema Frank Ribery baada ya kuinua kikombe hicho. "Tulikuwa na bahati leo. Nadhani ushindi huu utatusaidia na utatupatia motisha zaidi," akaongeza kusema Ribery.
Kiungo wa Chelsea, Ramires, alitolewa uwanjani dakika ya 85 kwa kuonyeshwa kadi nyekundu baada ya kumfanyia madhambi Mario Goetze wa Bayern. Hata hivyo vijana 10 wa Jose Mourinho walifunga bao la pili dakika ya tatu ya kipindi cha kwanza cha muda wa ziada kupitia Mbelgiji Eden Hazard. Hazard aliwachenga walinzi wawili wa Bayern katika wingi ya kushoto na kuvurumisha mkwaju uliopita mikono ya mlinda lango wa Bayern, Manuel Neuer, na kuutikisa wavu. Timu ya Pep Guardiola iliendelea kukidhibiti kindumbwendumbwe hicho, kama ilivyofanya wakati ilipokuwa ikiongozwa na kocha wa zamani, Jupp Heynckes, katika fainali ya Champions League miezi 15 iliyopita, lakini juhudi zao za kufunga mabao zilikwamishwa na kipa wa Chelsea, Petr Cech, aliyekuwa macho sana kila mara akiokoa mabao ambayo yalikuwa yaingie wavuni.
Pep 'ampepeta' Mourinho
Ilionekana kana kwamba Chelsea wangeshinda mpambano huo kwa mabao 2-1, hadi pale Javi Martinez wa Bayern, aliposawazisha sekunde chache tu kabla kipyenga cha mwisho kupulizwa kumaliza kipindi cha mwisho cha muda wa ziada. "Wanachukua kikombe lakini timu bora imeshindwa. Wapinzani wetu wamefunga magoli mawili na sisi pia tumefunga mawili. Lakini wamefunga penalti moja zaidi kuliko sisi. Ni wazi kabisa timu bora imepoteza mechi hii," amesema kocha wa Chelsea, Jose Mourinho, wakati wa mahojiano yake na Sky Sports.
"Kwangu mimi tulikuwa timu bora zaidi. Bayern walikuwa na dakika 15 katika kipindi cha pili ambazo walitawala mchezo na kuudhibiti mpira, lakini licha ya kuwa na wachezaji 10, tulicheza vizuri sana. Tumecheza dhidi ya mabingwa wa Ulaya na wachezaji wangu walikuwa timu bora - tuna sababu za kujivunia kuamini katika siku zijazo. Napendelea kusema tu kwamba timu bora imeshindwa na nitabaki na msimamo huo," akaongeza kusema Mourinho.
Akifurahia ushindi wake wa nane dhidi ya Mourinho katika michuano 16 iliyopita, Pep Guardiola amempongeza mtangulizi wake, Jupp Heynckes, aliyeiongoza Bayern kushinda mataji matatu msimu uliopita. "Nataka kumshukuru Jupp Heynckes kwa fursa ya kucheza katika fainali hii. Ni kwa sababu ya bidii yake kwamba tuko hapa."
Maoni na hisia tofauti
Guardiola ametofautiana na msimamo wa Mourinho kwamba timu bora imepoteza mechi hiyo. "Naamini timu bora ndiyo iliyoshinda. Sisi tulitengeneza nafasi nyingi za kufunga magoli. Chelsea ina wachezaji wenye uzoefu mkubwa kama vile Petr Cech, Frank Lampard, John Terry na Ashley Cole. Walikuwa na nafasi zao, lakini tulistahili kushinda." amesema kocha huyo wa Bayern.
Wakati huo huo, mlinda lango wa Chelsea, Petr Cech, amesema, "Tulitaka sana kushinda kombe hili na wao pia walitaka. Walilitafuta bao la kusawazisha na sisi tulikuwa tukiwazuia na kuimarisha kwa bidii safu yetu ya ulinzi. Inauma sana jinsi walivyofaulu kukomboa." Cech ameongeza kusema, "Kila mtu anaichukulia Bayern kama timu yenye nafasi nzuri ya kushinda Champions League msimu huu na kama timu bora duniani wakati huu, lakini tumeonyesha umahiri mkubwa, wakati mambo yalipokuwa yakituendea kombo."
Ni mchuano wa kwanza kuwania Super Cup kutochezwa Monte Carlo tangu mwaka 1997 na bila shaka ndio umekuwa wa kusisimua zaidi na wenye kumbukumbu nyingi kuliko michuano mingine yote. Pia ni fainali ya kwanza ya Super Cup ambapo mshindi amepatikana kupitia penalti.
Mwandishi: Josephat Charo/RTRE/DPAE
Mhariri: Caro Robi