1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern, Schalke zaduwazwa

26 Novemba 2014

Wanaongoza kundi lao na tayari wamefuzu, lakini kichapo cha Bayern cha mabao 3-2 dhidi ya Manchester City bado kilidhihirisha mchuano wa kusisimua. Schalke ilibamizwa 5-0 na Chelsea

https://p.dw.com/p/1Dtkb
Champions League Manchester vs Bayern München Aguero 25.11.2014
Picha: Alex Livesey/Getty Images

Hata baada ya kuutawala mchezo, Bayern walifungwa goli katikati ya kipindi cha kwanza. Mehdi Benatia alimwangusha Sergio Aguero katika eneo la hatari na refarii akamtimua uwanjani Mmorocco huyo na kuipa City penalty ambayo Aguero alisukuma wavuni.

Licha ya kufungwa, Bayern waliendelea kuudhibiti mchezo na Xabi Alonso akasawazisha kupitia free kick nje kidogo ya kijisanduku na kufanya mambo kuwa moja kwa moja. Muda mfupi baadaye Robert Lewandowski alifunga la pili kwa njia ya kichwa na kuwaweka vijana hao wa Pep Guardiola kifua mbele wakati wa kipindi cha mapumziko.

Champions League Schalke Chelsea John Terry Tor 25.11.2014
Chelsea walionyesha kabumbu safi katika uwanjani VeltinsPicha: Reuters/Wolfgang Rattay

City walijaribu bila kufua dafu kuona lango la Bayern lakini badaye Sergio Aguero akatumia fursa aliyopata na kufunga goli la pili baada ya Alonso kupiga pasi hafifu. Na mambo yalikuwa mabaya hata zaidi katika dakika ya mwisho wakati City walipopata bao la tatu na la ushindi baada ya Boateng kuzembea katika eneo hatari na Sergio Aguero akabusu nyavu Manuel Neuer asiwe na la kufanya.

Schalke yaduwazwa Gelsenkirchen

Huku akikabiliana na mwalimu wake wa zamani na klabu yake ya zamani, Roberto Di Matteo alikuwa an usiku mbaya kabisa wakati Cheslea ilipodhihirisha kila sababu ya umahiri wao, kwa kuwabamiza Schalke mabao matano bila jibu.

Kuanzia dakika ya mwanzo, Chelsea waliumiliki mchezo na goli la kwanza lilifungwa katika dakika tatu za kwanza kwa njia ya kichwa chake John Terry. Safu ya ulinzi ya Schalke ilikuwa mbovu, na washambuliaji wa Jose Mourinho wakaitumia vilivyo, huku Willian akisukuma wavuni bao la pili. Bao la tatu la Chelsea lilifungwa na mchezaji wa Schalke Jan Kirchhoff aliyepiga kichwa safi langoni mwake.

FC Barcelona vs. Real Madrid 25.10.2014
Lionel Messi aweka rekodi mpya katika Champions LeaguePicha: picture-alliance/dpa

Katika kipindi cha pili, Didier Drogba aliyeingia kama mchezaji wa akiba alifunga la nne wakati naye Ramires aambaye pia aliingia kama nguvu mpya akimaliza kazi kwa kuweka kichwa safi baada ya kuandaliwa krosi na Drogba.

Kwingineko Ulaya

Lionel Messi alivuja rekodi ya ufungaji magoli katika Champions League kwa kutikisa wavu mara tatu hapo jana katika ushindi wa Barcelona wa mabao manne kwa sifuri dhidi ya APOEL Nicosia. Messi sasa ana mabao 74 katika dimba hilo. Katika mechi nyingine za Kundi F, PSG iliizaba Ajax mabao matatu kwa moja, huku Zalatan Ibrahimovic aliyerejea kikosini baada ya kupona jeraha kufunga goli la pili muhimu.

Athletic Bilbao ilipata ushindi muhimu wa goli moja kwa sifuri ugenini dhidi ya Shakhtar Donetsk, lakini bao wako nyuma ya mabingwa hao wa Ukraine na pengo la points nne katika nafasi ya pili ya Kundi H. Porto inasalia kileleni baada ya kuibwaga BATE Borisov ugenini mabao matatu kwa bila. Katika kundi la Bayern, Roma walinyimwa ushindi mjini Moscow baada ya bao la dakika ya mwisho ya mchezo kuwasawazishia wenyeji na kumaliza mchezo katika sare ya bao moja kwa moja.

Mwandishi. Bruice Amani/afp/DW
Mhariri: Josephat Charo