Bayern yatengana na kocha Carlo Ancelotti
29 Septemba 2017Mabingwa wa Bundesliga Bayern Munich walidhalilishwa kwa kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya paris saint-Germain katika mchezo wa pili wa makundi wa Champions League siku ya jumatano, na klabu hiyo ilichukua hatua za haraka kumfuta kazi kocha Ancelotti siku ya Alhamis.
Baada ya kubugia kipigo cha mabo 2-0 dhidi ya Hoffenheim na kuachia ushindi wakati wakiongoza kwa mabao 2-0 nyumbani dhidi ya VFL Wolfsburg, hata kiwango cha Bayern katika Bundesliga kilikuwa mbali na chake cha kawaida cha udhibiti katika wiki za hivi karibuni.
Wakati klabu hiyo imebakia katika nafasi ya tatu nyuma ya Hoffenheim na viongozi Borussia Dortmund , minong'ono ya kutokuwa na amani ndani chumba cha kuvalia wachezaji iliongeza mbinyo kwa Anceloti.
Akikabiliwa na ukosoaji kutoka kwa mashabiki na vyombo vya habari kwa kushindwa kumtumia vizuri Thomas Mueller , uhusiano wa Ancelotti na wachezaji kama Robert Lewandowski, Arjen Robben na frank Ribery pia unaripotiwa kuwa uliathirika.
Wakati Sagnol anachukua hatamu za uongozi kwa muda, Bayern itabidi kuimarisha msimu wake wakati wanasafiri kwenda kupambana na Hertha Berlin.
Kikosi cha Carlo Ancelotti
Ancelotti alikosolewa vikali kwa jinsi alivyoteua kikosi chake kilichopambana na PSG, na Mats Hummels , Robben, Ribery na Jerome Boateng wanatarajiwa kurejea katika kikosi cha kwanza dhidi ya Hertha.
"Natarajia maendeleo chanya kutoka katika timu, na bila shaka nia ya kucheza vizuri," amesema bosi wa klabu hiyo Karl_heinz Rummenigge baada ya kutupwa nje Carlo Ancelotti.
Bayern inahitaji kocha mpya wa muda mrefu, na kuna fununu kwamba baada ya mapunziko ya michezo ya timu ya taifa viongozi watafikia uamuzi wa kumleta mmoja kati ya makocha ambao wanazungumziwa sana kumrithi Carlo Ancelotti.
Majina yanayotajwa kuchukua nafasi hiyo ni pamoja na kocha wa hivi sasa wa TSG Hoffenheim , Julian Nagelsmann , na Thomas Tuchel kocha wa zamani wa Borussia Dortmund.
Tatizo la nagelsmann ni kwamba bado ana mkataba na Hoffenheim, lakini Thomas Tuchel hana kazi kwa sasa na anaweza kupatikana mara moja.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe