Bayern yawakwaruza Arsenal
20 Februari 2013Katika mchuano mwengine, Porto walipata ushindi wa goli moja kwa sifuri dhidi ya Malaga. Mabingwa mara nne wa Ulaya, Bayern, walichukua uongozi katika uwanja wa Emirates kufuatia magoli ya Toni Kroos na Thomas Mueller. Arsenal walijibu baada ya kipindi cha pili kuanza kupitia mchezaji wa zamani wa Bayern Lukas Podolski, lakini mshambuliaji raia wa Croatia Mario Mandzukic akamudu kufunga goli la tatu.
Goli la Podolski ndilo lililokuwa la kwanza kwa vijana hao wa mkufunzi Jupp Heynckes mwaka huu, na mara ya kwanza katika dakika 664 mlinda lango Manuel Neuer kufungwa goli langoni. Heynckes ameusifu mchezo wa kikosi chake na hasa akammiminia sifa mshambuliaji wake Mario Mandzukic.
Miamba hao wa Bundesliga ambao wanajaribu kurekebisha kichapo walichopata kutoka kwa Chelsea kupitia mikwaju ya penalti katika fainali ya mwaka jana, waliwafedhehesha Arsenal kwa dakika 45 za kwanza na hata ingawa walififia katika kipindi cha pili, wanapigiwa upatu kufuzu katika robo fainali. Arjen Robben amesema baada ya mechi kwamba wameimarika ikilinganishwa na mwaka jana. Na wamepiga hatua kubwa ya kufika robo fainali.
Mkufunzi wa Arsenal anayekumbwa na shinikizo Arsene Wenger aliongeza kuwa ukweli ni kwamba wana mlima mkubwa wa kukwea lakini watajaribu kufanya lisilowezekana liwezekane. Kwamba watakwenda Ujerumani kucheza jinsi wanavyocheza nyumbani na kujaribu kubadilisha matokeo.
Kiungo wa Arsenal Jack Wilshere alimtetea kocha wake akisema ni jukumu la wachezaji kufanya wanachoambiwa uwanjani, na kwamba Wenger amefanya kazi nzuri kwa miaka 16 iliyopita akiwa katika klabu hiyo.
Na nchini Ureno, mabingwa mara mbili wa Ulaya walipata ushindi dhidi ya Malaga, katika juhudi za klabu hiyo ya Ureno kufika robo fainali kwa mara ya kwanza katika miaka mitano. Kiungo Mreno Joao Moutinho alitikisa wavu goli la pekee katika dakika ya 56. Baada ya mechi sita za mkondo wa kwanza katika awamu ya mchujo, Porto ndiyo timu pekee ambayo haijashinda mchuano wake wa nyumbani.
Mkufunzi wa Malaga raia wa Chile Manuel Pellgrini amesema kitu cha muhimu ni kusubiri kipenga cha mwisho baada ya mchuano wa mkondo wa pili. Amesema wana uwezo wa kubadilisha mambo katika mkondo wa pili nyumbani katika uwanja wa La Rosaleda.
Katika mechi za leo, AC Milan watakuwa wenyeji wa Barcelona, wakati Galatasaray wakiwa wenyeji wa Schalke 04. Schalke wana kibarua dhidi ya Galatasaray ambao wamekiimarisha kikosi chao kwa kuwaleta Wesley Schneider na Didier Drogba. Schalke wamepigwa jeki na kurejea kwa Mholanzi Klaas-Jan Huntelaar. Hata hivyo watakosa huduma za wachezaji Atsuto Uchida, Lars Unnerstall, Ibrahim Afellay, Kyriakos Papadopoulos, Ciprian Marica na Christoph Moritz.
Mabingwa mara saba AC Milan na Barca ambao walikutana katika awamu ya makundi na robo fainali msimu uliopita, wanakutana tena katika uga wa San Siro huku Lionel Messi na wenzake wakipigiwa upatu kutawala.
AC Milan watakosa huduma za Mario Balotelli ambaye haruhusiwi kucheza katika dimba hili wka sababu aliwachezea Manchester City kabla wabanduliwe nje.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters/DPA
Mhariri: Sekione Kitojo