1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BEIJING: Baraza la usalama la Umoja wa mataifa lakaribia kuafikiana juu ya vikwazo vya kuiwekea Korea ya kaskazini

13 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CD3K

Marais wa Uchina na Korea ya kusini wamekubaliana Baraza la usalama la Umoja wa mataifa lichukuwe hatua zinazostahili dhidi ya Korea ya kaskazini kufuatia jaribio lake la kuripua bomu la kinyuklia. Hata hivyo marais wa Uchina Hu Jintao na mwenzake wa Korea ya kusini Roh Moo-Hyun hawakutoa maelezo zaidi.

Roh Moo-Hyun, amewasili mjini Beijing nchini Uchina kwa mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo. Marekani imetaka wapigie kura leo azimio la Umoja wa mataifa la kuiwekea vikwazo Korea ya kaskazini. Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa mataifa John Bolton, alisema baada ya mkutano kumalizika kwamba wanakaribia kufikia makubaliano juu ya swala hilo:

´´Unajua, ni jambo zuri sana. Wajumbe wa baraza wamesema msimamo wa Korea ya kaskazini hadi sasa unapelekea kila mmoja kuwa na hisia kwamba ni budi Baraza la usalama lichukuwe hatua kali. Kwa hiyo ninafikiri ikiwa Korea ya kaskazini inahisi kuwa imefanikiwa kuzitisha nchi zingine katika baraza la usalama, imekosea´´

John Bolton aliongeza kutetea hatua ya kuiwekea Korea ya kaskazini vikwazo kwa kusema:

´´ Nina uhakika Teheran inafuatilia kile tutakachokiamua juu ya azimio dhidi ya Korea ya kaskazini. Ninaamini wanafuatilia kwa karibu zaidi´´

Hata hivyo, mswada wa vikwazo ambao umefanyiwa marekebisho, haupendekezi tena vikwazo vya silaha ila umebakiza kupekuliwa meli zitakazoelekea au zitakazotoka Korea ya kaskazini.