Beijing. Condoleeza aitaka China kuwajibika katika vikwazo dhidi ya Korea ya kaskazini.
20 Oktoba 2006Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Condoleezza Rice ameitaka China kusaidia utekelezaji kamili wa azimio la umoja wa mataifa dhidi ya Korea ya kaskazini kutokana na jaribio lake la silaha za kinuklia hapo Oktoba 9.
Baada ya mkutano wake na waziri wa mambo ya kigeni wa China Li Zhaoxing mjini Beijing, Rice amesema amejadiliana na waziri huyo jinsi China inavyoweza kutekeleza hatua hiyo, hususan katika upekuzi wa mizigo inayotoka na kwenda Korea ya kaskazini.
China ni mshirika mkubwa wa kibiashara na Korea ya kaskazini na itakuwa na jukumu kubwa katika utekelezaji wa vikwazo hivyo vya umoja wa mataifa katika usafirishaji ndani na nje ya nchi hiyo.
Vikwazo hivyo vinalenga kuizuwia Korea ya kaskazini kusambaza silaha za kinuklia. Li amewaambia waandishi wa habari baada ya mkutano huo kuwa China inalenga kutekeleza wajibu wake kama inavyotakiwa katika azimio hilo. Rice yuko katika kituo chake cha tatu katika ziara yake ya mataifa ya Asia ili kujadili jibu la jumuiya ya kimataifa dhidi ya jaribio la silaha za kinuklia lililofanywa na Korea ya kaskazini.