BEIJING: Marekani yafanya mazungumzo na Korea Kaskazini
19 Desemba 2006Mazungumzo ya mataifa sita kuhusu mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini yanaendelea leo mjini Beijing China. Marekani na Korea Kaskazini zimeanza mazungumzo kandoni mwa mkutano huo kuhusu vikwazo vya kifedha vilivyowekwa na Marekani dhidi ya utawala wa Pyongyang.
Mjumbe wa Marekani katika mazungumzo hayo, Chrisptopher Hill, amekutana ana kwa ana na mwenzake wa Korea Kaskazini, Kim Kye-Gwan.
Akizungumza kuhusu msimamo wa mataifa yanayoshiriki katika mazungumzo ya mataifa sita, Christopher Hill, amesema,
´Hakuna nchi itakayokubali Korea Kaskazini imiliki silaha za kinyuklia. Korea Kaskazini inahitaji shule, vituo vya afya, barabara, viwanja vya ndege, wanahitaji vitu vingi. Wanahitaji umeme na wala hawahitaji silaha za kinyuklia.´
Korea Kaskazini jana iliitaka serikali ya Washington ifutilie mbali vikwazo vya kifedha na kutaka vikwazo vya Umoja wa Mataifa ilivyowekewa baada ya kufanya jaribio la zana zake za nyuklia viondolewe.