BEIJING.Marekani yapongeza hatua ya Korea Kaskazini
14 Februari 2007Korea Kaskazini imekubali kuchukua hatua zitakazo iwezesha nchi hiyo kusimamisha mpango wake wa nyuklia baada ya kufikiwa makubaliano ya kupokea msaada wa dola milioni 300.
Rais George Bush wa Marekani amepongeza makubaliano hayo na amesema kwamba hatua hiyo itaiwezesha Pyongyang kuacha mpango wake wa nyuklia.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleeza Rice pia ameyakaribisha makubaliano hayo yaliyofikiwa katika mazungumzo ya pande sita yaliyofanyika mjini Beijing nchini China.
Pyongyang imeahidi kuanza hatua ya kwanza na hatimaye kusimaisha kabisa shughuli katika kinu chake kikuu cha kutengeneza nyuklia.
Marekani na Japan zimesema kuwa zitaanzisha uhusiano wa karibu na Korea Kaskazini.
Katika mkubaliano hayo Korea Kaskazini inahitajika kuanza hatua ya mwanzo ya kusimamisha mpango wake wa nyuklia katika muda wa siku 60.
Mazungumzo ya pande sita yalianza mjini Beijing alhamisi iliyopita.