1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bima ya afya yaahirishwa ?

3 Januari 2007

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wametuwama leo juu ya mada 2: kuahirishwa mjadala juu ya mswada wa bima ya afya na dai la waziri wa ndani kutaka sheria ya kutungua ndege zilizotekwanyara.

https://p.dw.com/p/CHU4

Kutokana na shinikizo la vyama vya CDU/CSU katika serikali ya muungano ya Ujerumani,mswada wa maguezi ya bima ya afya upitishwe mwezi ujao na sio huu.Kwanza hasa chama cha CSU kilichohoji baadhi ya nguzo muhimu zinazosimamia mageuzi hayo.

Gazeti la Financial Times la Ujerumani limepitisha hukumu kali juu ya mkasa unaopita sasa.Lauliza:

“Je, mwaka 2007 kwa serikali ya muungano wa vyama vikuu utageuka mwaka wa konokono ?....

Mpango wa mageuzi wa Kanzela Angela Merkel umekwama na unazorota.Kwani hata kwa kupitisha zaidi wakati ,haitasaidia kitu kuyabadili mageuzi mabaya kuwa mazuri.Zaidi ni uwwezekano ni mkubwa kwamba mwishoe hapa hakutakua na matengenezo bali uharibifu zaidi….

Bibi Merkel,ingekua busara laiti angesalia na siasa zake za kupiga hatua ndogo-ndogo za mageuzi-mfano kuachana kabisa na mpango wake wa mfuko wa bima ya afya ulioingia dosari….”

Gazeti la Kölnische Rundschau likichambua kwa msimamo sawa na huo lauliza nalo:

“kwa mara ya ngapi sasa maguezi haya makubwa ya bima ya afya yanaahirishwa ?Vyama vya CDU/CSU vinataka kuahirisha kuanza kazi mpango wa mfuko wa bima ya afya uliotungwa na mwanasiasa wa chama cha SPD Bw.Lauterbach.Dakika za mwisho wanasiasa wa vyama hivyo 2 wanajifanya kana kwamba havikushiriki katika kuutunga mpango huo.

Vyama hivyo vya CDU/CSU vitajiharibia binafsi ikiwa mpango huo vitauachia upite bila kuufanyia mageuzi.Lakini, bei gain mshirika wao serikalini-SPD atadai kwa kuviridhia ?”

Ama gazeti la LÜBECKER NACHRICHTEN linamurika kwa mara nyengine tena mchango wa chama cha CSU na mwenyekiti wake waziri-mkuu wa Bavaria Bw.Stoiber:

Laandika kwamba, Edmund Stoiber ameitilia serikali kitumbua chake mchanga.

Amelenga hapo kuwapa satua wabunge wake katika Bunge la shirikisho.Msimamo aliouchukua Bw.Stoiber ni wa kutaka kupendeza kwa wafuasi wake na mtu athubutu hata kueleza hiyo si tabia nzuri alioionesha.

Lakini hata ikiwa hakuonesha nia njema hapo, mtu yafaa kutoa shukurani kwa kiongozi huyo wa CSU.Kwani, misukosuko yake ya karibuni inamurika tena dosari za mageuzi haya ya bima ya afya.Pengine, ingelikua bora, mageuzi haya yangetupwa kabisa katika debe la taka.”

Akitugeuzia mada, waziri wa ndani wa Ujerumani kutoka chama ndugu cha CDU Bw.Wolfgang Schauble,amekataliwa mpango wake wa kutaka kuziangusha ndege zilizotekwanyara na magaidi kwa makobora .Hata wahariri hawaafikiani nae.

Gazeti la OSTSEE ZEITUNG kutoka Rostock laandika :

„Wapinzani wamejifunga kibwebwe kupambana vikali na sheria mpya anazotaka kutunga Bw.Schauble kulinda anga la Ujerumani.Kwani zinatoa sura ya kumpa leseni ya kuuwa watu wasio na hatia.

Kwani yafaa kuuliza iwapo inastahiki kuua watu wasio na hatia waliomo ndani ya ndege iliotekwanyarta ili kuepusha msiba wa kutekwa nyara ndege ?

Hoja ya kwanza kufyatua risasi ndipo baadae uulize haitakikani.Kwahivyo, hata waziri huyu wa mambo ya ndani na serikali ya ujerumani afaa kuheshimu hukumu ya Mahkama Kuu ya Ujerumani.

Nalo gazeti la HEILBONNER STIMME linatuzindua juu ya hukumu ya karibuni juu ya swali hili iliokatwa na Mahkama Kuu ya katiba mjini Karlsruhe:Linasema:

„Bw.Schauble anadharau mapendekezo ya mahkama hiyo.Mahakimu wake kiasi mwaka mmoja tu uliopita, walibatilisha sheria ya ulinzi wa anga la Ujerumani.

Hapo walilikataa pia ombi la Bw.Schauble kufyatua risasi kuziangusha ndege za abiria zilizotekwa nyara.Hukumu iliweka dhahiri-shahiri kwamba si haki katika kunusuru maisha ya watu fulani kutoa mhanga maisha ya wengine.

Gazeti la MANNHEIMER MORGEN linadhani kwamba, waziri huyo wa mambo ya ndani hakusudii sana hapo sheria ya ulinzi wa anga kuliko anavyokusudia sera nzima mpya za usalama.

Anataka kulifanya Bundeswehr sio kubakia linatumika kwa kazi za uokozi yanapozuka mafuriko au kuweka usalama anapozuru baba mtakatifu nchini Ujerumani,bali kuwa chombo cha kupambana na ugaidi.

Ili aweze kufanya marekebisho yatakayo katika sheria za usalama atahitaji kuungwamkono na chama cha SPD-mshirika serikalini.

Sungura huyu mkongwe anajua vyema kucheza karata zake:Dai makuu tena mengi –kama vile kuzitungua ndege zilizotekwanyara na magaidi,ili alao uponee kupata machache utakayo-yaani kuona jeshi la Ujerumani, latumika katika usalama wa ndani ya nchi hii.