Bosi wa Bayern aiunga mkono Dortmund kuhusu Auba
19 Januari 2018Aubameyang kwa mara nyingine tena ameenguliwa katika kikosi cha Dortmund katika mchezo wa leo Ijumaa wa ligi dhidi ya Hertha Berlin baada ya pia kusitishwa kucheza na kocha mkuu wa Borussia Peter Stoeger katika mchezo uliokwenda suluhu nyumbani dhidi ya Wolfsburg.
Mchezaji huyo nyota wa Borussia Dortmund mwenye umri wa miaka 28 amepachika wafuni mabao 13 katika michezo 15 ya ligi msimu huu, akifunga mara 21 katika michezo 23 katika mashindano yote.
Hata hivyo , alipewa karipio la utovu wa nidhamu kwa mara ya tatu katika muda wa miezi 16 kwa kushindwa kuhudhuria mkutano wa timu mwishoni mwa juma lililopita.
Baba yake mzazi na ambaye ni wakala wake anaripotiwa kuwapo mjini London akijaribu kutayarisha hatua za uhamaji kwenda Arsenal kwa kijana wake, lakini Heynckes amesema Dortmund wako sahihi kwa kumuacha mfungaji wao huyo nyota.
Aubameyang hatabiriki
Kocha huyo wa Bayern mwenye umri wa miaka 72 amesema anasikitishwa sana hususan baada ya Ousmane Dembele kususia mazowezi ya timu Agosti mwaka jana katika juhudi za kuilazimisha Dortmund kumuuza kwa Barcelona.
"Kitu kinachotokea Dortmund kuhusu Dembele na Aubameyang unahitaji kukiangalia kwa undani zaidi," Heynckes alisema mjini Munich leo Ijumaa(19.01.2018)
"Nafikiri kwamba klabu yoyote inapaswa kufikiri mara mbili juu ya kumchukua mchezaji kama huyo na naweza kusema kwa kweli, sitamkubali mchezaji kama huyo.
"Bado ni mchezo wa timu nzima na hakuna nafasi kwa hayo.
"Ni lazima tuwe waangalifu kwamba mashabiki hawatukimbii katika wakati fulani."
Heynckes amesema hawezi kufikiria hali kama hiyo inayoweza kumhusu mmoja kati ya wachezaji wake katika Bayern.
"Huwezi kusema haitaweza kutokea Bayern , lakini nasema wazi kabisa siwezi kufikiria kitu kama hivyo kutokea.
"Wachezaji wana wajibu wao, wana wajibu mkubwa kwa klabu zao, kwa hiyo haitoshi tu kuangalia salio lako katika benki mwishoni mwa mwezi."
Dortmund iko nafasi ya nne katika msimamo wa ligi wakati Bayern inaanza michezo wa mwishoni mwa juma ikiwa na pointi 13 zaidi ya timu iliyoko karibu yake RB Leipzig kabla ya pambano la siku ya Jumapili nyumbaji dhidi ya Werder Bremen.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe